Msako mkali polisi watano wakiuawa na magaidi Boni
MSAKO mkali umeanzishwa kuwatafuta magaidi wa Al-Shabaab walioua maafisa watano wa polisi wa kitengo cha operesheni maalumu (SOG) na wengine wanane kujeruhiwa vibaya.
Shambulizi hilo lilitekelezwa Jumatano katika eneo la Lehelo, karibu na Janjana kwenye msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu.
Kulingana na ripoti ya polisi kutoka kambi ya Nyangoro, tarafa ya Witu, Lamu, maafisa waliouawa walikuwa miongoni mwa makumi ya walinda usalama waliokuwa wamesambazwa kushika doria na kuendeleza operesheni ya kuwasaka magaidi waliokuwa wameonekana maeneo hayo ya Lehelo, Janjana na viunga vyake.
Baada ya siku mbili za msako, maafisa walikutana ana kwa ana na magaidi wengi wa Al-Shabaab waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari.Ripoti hiyo inaeleza kuwa ufyatulianaji mkali wa risasi kati ya walinda usalama na Al-Shabaab ulianza na kupelekea vifo vya polisi watano na wengine wanane kujeruhiwa vibaya.
Inaaminika kuna magaidi waliouawa katika makabiliano hayo wengi wakijeruhiwa, ingawaje idadi yao haikubainika mara moja.
“Timu ya polisi wa kitengo cha operesheni maalumu (SOG) kilisambazwa eneo la Janjana na Lehelo ndani ya msitu wa Boni kusaidia kupiga doria za kuwatafuta maadui. Baada ya siku mbili timu ilipambana ana kwa ana na magaidi hao hali iliyopelekea makabiliano makali. Matokeo yalikuwa kwamba polisi watano walikufa ilhali wanane wakijeruhiwa vibaya.Waliojeruhiwa walipelekwa Manda na kisha baadaye Nairobi,” ikasema ripoti hiyo ya polisi.
Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Lamu, Bw Kispang Changach pia alithibitisha tukio hilo Ijumaa na kusema kuwa operesheni kali ya kuwasaka magaidi inaendelea.“Ni masikitiko kwamba tuliwapoteza maafisa wetu ilhali wengine walijeruhiwa wakati wakitekeleza majukumu yao juzi. Tumeanzisha operesheni kali ya kuwatafuta maadui. Hatutachoka,” akasema Bw Changach.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo walieleza kutoridhishwa kwao na hulka ya Al-Shabaab kujitokeza kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu kila baada ya muda kushambulia, kujeruhi na hata kuua walinda usalama na raia.
“Tuko na operesheni ya kiusalama msituni Boni ambayo imedumu kwa karibu miaka kumi sasa. Tuambiwe endapo hiyo operesheni yafanya kazi au la. Kwa nini fedha nyingi zachomeka msituni walinda usalama wakipigana na Al-Shabaab ilhali bado maadui wajitokeza kushambulia na hata kuua? Hatufurahii kamwe,” akasema Bw Ali Tenee, mkazi wa msitu wa Boni.
Shambulio na mauaji ya polisi watano na kujeruhiwa kwa wengine wanane linajiri siku mbili tu baada ya watu watano wachimba migodi kuuawa kwa kupigwa risasi kaunti ya Mandera Jumanne asubuhi.
Wawili wengine waliachwa na majeraha mabaya.Aprili 5 mwaka huu, polisi wa kitengo cha kukabiliana na ghasia (GSU) walitibua jaribio la Al-Shabaab kuvamia na kuilipua kambi yao iliyoko kijiji cha Basuba, msitu wa Boni, Lamu Mashariki.
Kwenye shambulio hilo la usiku, Al-Shabaab pia walijaribu kuvamia kijiji cha Basuba lakini wakakabiliana vikali na askari wa akiba (NPR) waliowashinda nguvu na kutokomea kwenye msitu wa Boni.
Hakuna aliyeuawa au kujeruhiwa kwenye makabiliano hayo.Machi 15, 2025, karibu magaidi 150 wa Al-Shabaab waliojihami kwa silaha hatari walivamia kijiji cha Mangai majira ya jioni ambapo waliwakusanya watu mahali pamoja na kuwahubiria mafundisho ya itikadi kali.
Baadaye waliwagawia matunda ya tende kama zawadi ya Ramadhani kabla ya kutorokea msitu wa Boni.Pia hakuna aliyeuawa ama kujeruhiwa kwenye uvamizi huo wa majira ya saa kumi na mbili unusu jioni.