Msiwe na pupa yoyote ya kuingia mkataba na Ruto, Gavana Orengo aonya ODM
GAVANA wa Siaya James Orengo ambaye ni mshirika wa karibu wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga ameonya chama hicho na wakazi wa Nyanza kutokuwa na haraka ya kutia saini mkataba wa kisiasa na Rais William Ruto, akisema huenda kikajiangamiza kisiasa.
Tahadhari yake inajiri siku chache kabla ya tangazo linalotarajiwa kutolewa na Bw Odinga kuhusu mwelekeo wa kisiasa huku wengi wakimtarajia atangaze kuungana rasmi na Rais Ruto kwa kudai asilimia 50 ya serikali.
Gavana wa Siaya, ambaye alihutubia waombolezaji katika kijiji cha Imbayi eneobunge la Alego Usonga katika mazishi ya marehemu Mama Leah Obiero, mamake ripota wa masuala ya siasa wa kampuni ya Nation Media (NMG), Justus Ochieng, alisema kuharakisha makubaliano ya aina yoyote kutakuwa na madhara.
“Ninaomba tuchukue muda na kuzingatia chochote kitakachotokana na mashauriano. Huwezi kuwa mtu anayeharakisha kunyakua fursa yoyote ya kisiasa inayojitokeza,” akasema.
Aliendelea: “Nazungumza kama mkongwe katika siasa za Kenya na ninaposema tusikimbilie mambo, ninamaanisha ninachosema. Nilifanya kazi enzi za rais mwanzilishi Jomo Kenyatta na Daniel Moi; Hatukuwa na wakati rahisi naye, rais wa tatu Mwai Kibaki na Rais wa wa nne Uhuru Kenyatta, kwa hivyo ninaelewa siasa vizuri zaidi,” alisema.
Alitoa wito kwa uongozi wa ODM kutafakari matukio ya awali yanayofanana na ya wakati huu.“Ningependa kuwatahadharisha baadhi ya viongozi vijana waliochaguliwa ambao wanakimbilia kunyakua fursa za kisiasa.
“Wanapaswa kuuliza baadhi ya wana wetu waliokimbilia fursa kama hizo kama marehemu Oloo Aringo (Alego Usonga), Odongo Omamo na Robert Ouko,” akaongeza mkuu huyo wa kaunti.
Pia alieleza kuwa mashauriano yanayoendelea ambayo Waziri Mkuu huyo wa zamani anafanya yafanywe kwa umakini bila kuharakisha chochote. “Wacha mashauriano na watu yaendelee na ninaamini tutakuwa na njia sahihi ya kushughulikia mambo ya sasa,” aliongeza.
Maoni ya Bw Orengo yanajiri siku chache baada ya kuongoza timu ya viongozi waliokutana na Bw Odinga katika mkutano wa mashauriano katika afisi yake Siaya.
Maoni yake, hata hivyo, yalionekana kinyume na yale ya mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi ambaye alihimiza uongozi wa chama cha ODM kutorudi nyuma katika mkataba wa ushirikiano wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na Bw Odinga.