Mtangazaji wa zamani Salim Swaleh nje kwa dhamana katika kesi ya ulaghai
MKURUGENZI wa masuala ya mawasiliano Salim Swaleh, katika afisi ya Waziri mkuu Musalia Mudavudi aliyekamatwa Jumapili na kuzuiliwa kwa sakata ya Sh5.8 milioni za ujenzi wa viwanja ameachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh400,000.
Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi aliwaachilia Swaleh na wenzake watano Michael Otieno Japolo, Terry Kemunto Sese, Daniel Omondi Gogo, John Musundi Wabomba na James William Makoha.
Bw Ekhubi alisema upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi ulio na mashiko ya kisheria kuwezesha korti kuwanyima dhamana.
Bw Ekhubi alisema sheria hairuhusu mshukiwa kunyimwa dhamana endapo hakuna sababu maalum za kuwezesha mahakama kutwaa haki zake.
Akiwaachilia sita hao wanaodaiwa kuwapunja wawekezaji Dola za Marekani, Bw Ekhubi aliwaamuru wawasilishe pasipoti zao kortini.
Pia aliwaagiza wasivuruge uchunguzi na kuwataka wapige ripoti kwa afisa anayechunguza kesi hiyo hadi mahojiano yakamilishwe.
Bw Ekhubi alitenga kesi hiyo itajwe Julai 7, 2024 kwa maelezo zaidi.
Polisi walielezwa waendelee na uchunguzi wao huku washukiwa wakiwa nje kwa dhamana.
Bw Ekhubi alitupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) la kuwataka washukiwa hao sita wazuiliwe kwa siku 14 ili mashahidi kutoka Dubai na Afrika Kusini waandikishe taarifa.
“Hakuna ushahidi uliowasilishwa kwamba washukiwa wakiachiliwa watatatiza polisi kuandikisha taarifa za mashahidi wakuu kutoka Dubai na Afrika Kusini,” Bw Ekhubi alisema.
Swaleh na wenzake watano ambao ni wafanyabiashara walitiwa nguvuni Jumapili baada ya wawekezaji wawili kutoka Dubai na Afrika Kusini kulalama walipunjwa Dola za Marekani (USD)45,000 (Sh5,850,000) kupewa zabuni ya ujenzi wa viwanja viwili vya michezo vya kusakatia kandanda wakati wa michezo ya Afcon 2027.
Uchunguzi kutapakaa kutoka Kenya hadi UAE
Michezo hii ya Afcon, hakimu alielezwa, itachezewa nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.
Akiomba washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 14, afisa mkuu anayechunguza kesi hiyo Inspekta Nicholas Njoroge alisema uchunguzi wa kesi hii utatapakaa kutoka Kenya hadi Jumuia ya Milki za Uarabuni (UAE-Dubai) na Afrika Kusini.
“Mwanakandarasi mkuu aliyehusika anaishi Dubai na mwingine yuko Afrika Kusini. Itabidi polisi wasafiri hadi nchi hizo kurekodi taarifa za mashahidi. Polisi wanahitaji muda kusafiri,” Insp Njoroge alimweleza hakimu.
Afisa huyo alisema uchunguzi huu utashirikisha idara mbali mbali za serikali kama vile Afisi ya msajili wa Makampuni katika afisi ya mwanasheria mkuu,Wizara za Michezo, Wizara ya Usalama wa Ndani na asasi kadhaa za serikali.
“Endapo Swaleh ambaye yuko na ushawishi mkubwa ataachiliwa atavuruga uchunguzi,” Insp Njoroge alisema huku akiomba ombi la polisi likubaliwe.
Alisema katika muda huu wa siku 14 uchunguzi wa pamoja katika mataifa hayo ya ng’ambo utafanywa kabla ya Swaleh na wenzake watano kushtakiwa rasmi.
Hata hivyo, mawakili Shadrack Wambui, Sam Nyaberi na Danstan Omari waliomba hakimu awaachilie washukiwas hao kwa dhamana ya Sh200,000 kwa vile serikali haijawasilisha sababu tosha za kuwezesha mahakama iamuru wazuiliwe kwa siku 14.
“Insp Njoroge amekiri hana sababu maalum za kuwezesha mahakama kuagiza Swaleh na wenzake kuzuiliwa siku 14. Hakuna uhalifu umethibitishwa walifanya,” Bw Omari alisema.
Mawakili wengine Wambui na Nyamberi walisema washukiwa hawawezi kuzuilia polisi kuwahoji mashahidi Dubai na Afrika Kusini
Akisisitisha washukiwa wazuiliwe siku 14, Insp Njoroge alisema walalamishi walishawishiwa wafike katika afisi ya Mudavadi na kufanya mashauri kuhusu ujenzi wa viwanja hivi viwili.
“Baada ya kumaliza mashauri katika afisi ya Mkuu wa Mawaziri aliye pia Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni walalamishi walifahamishwa watafululiza moja kwa moja hadi Wizara ya Usalama wa Ndani na Wizara ya Michezo. Katika kipindi hiki walalalamishi walitakiwa watoe Sh5.8m za kusajiliwa,” Insp Njoroge alisema.
Pia alisema masuala ya kidiplomasia yatahitajika katika uchunguzi huu na kwamba muda wa kutosha unahitajika.
Afisa huyo alisema Bw Swaleh aliruhusu mashauri ya mkutano na wawekezaji hao ufanywe katika afisi ya Mudavadi.
Mahakama ilielezwa Japolo alijifanya ndiye mwenyekiti wa idara ya Serikali ya uuzaji na upokeaji wa zabuni na kandarasi rasmi za serikali.
Japolo , mahakama iliambiwa, aliahidi kuharakikisha utiwaji sahihi zabuni hiyo haraka.
Hivyo basi walalamishi walielezwa walipe USD45,000 (KSh5,850,000) ndipo washinde zabuni hiyo.