Mtoto asimulia kortini jinsi babake mzazi alimwandaa kwa kifo Shakahola
MTOTO aliyenusurika kifo kwenye mfungo wa mauti katika msitu wa Shakahola amesimulia mbele ya mahakama jinsi babake alivyomwandaa kwa kifo.
Shahidi huyo alisimulia jinsi alivyovalishwa mavazi maalum kujiandaa kufa huku mshukiwa mkuu wa kuongoza dhehebu hilo potovu, Paul Mackenzie, akiwahimiza waumini wake kufunga kula na kunywa hadi wafe.
Alieleza jinsi ndugu zake watatu walivyoaga dunia mmoja baada ya mwingine, huku wazazi wao wakiwashawishi kuwa ndiyo njia pekee ya kwenda mbinguni na kukutana na Mungu.
“Baba yangu aliniagiza nivae nguo hizo na kunifahamisha zilikusudiwa kwa kifo changu. Kisha tukanyimwa chakula kwa siku nane,” mtoto huyo alisema alipokuwa akihojiwa na mawakili wa serikali Anthony Musyoka, Jami Yamina na Persi Bosibori.
Shahidi huyo alijawa na majonzi alipokuwa akisimulia masaibu yake y a kuhuzunisha katika msitu huo, hivyo kuilazimu mahakama kusitisha vikao vyake kwa muda mara kwa mara ili kumruhusu mtoto huyo kutulia.
“Baba yangu alinikabidhi nguo hizo na kuniahidi mahali mbinguni ikiwa nitaangamia kwa njaa,” mtoto huyo alisema.
Suruali nyeupe na fulana ya samawati aliyodaiwa kupewa mtoto huyo ziliwasilishwa kama ushahidi mahakamani.
Shahidi huyo alimweleza Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Mahakama ya Shanzu, Bi Leah Juma, kwamba hawakuwa wanaenda shuleni walipoishi katika msitu huo.
Aliieleza mahakama kuwa yeye na ndugu zake walipelekwa msituni na baba yao, huku mama yao akijiunga nao baadaye na kujifungua mtoto mwingine huko.
Alisema kuwa familia yao ilikuwa ikiishi katika kijiji cha Bethlehemu ndani ya Shakahola.
“Kwa kawaida tulihutubiwa na Bw Mackenzie ambaye pia alikuwa akijulikana kwa jina ‘Mtumishi’,” alisema mtoto huyo wakati akihojiwa na mawakili wa Mackenzie, Bw Lawrence Obonyo na Bw Chacha Mwita.
Alikumbuka kuona mikusanyiko msituni lakini hakukumbuka maudhui ya hotuba zilizotolewa kwa waumini hao.
“Mackenzie alikuwa akisema watu wafunge, na kwa sababu hiyo tulinyimwa chakula na wazazi wetu,” alisema mtoto huyo.
Zaidi ya hayo, mtoto huyo alifichua kuwa babake aliondoa miili ya ndugu zake nyumbani baada ya kuaga dunia kutokana na njaa.
“Walizikwa kwenye kaburi karibu na nyumbani kwetu. Mtumishi alikuwepo na akasema watu waendelee kufunga,” alisema mtoto huyo, ambaye aliokolewa na babu yake na maafisa wa polisi kutoka msituni.
Wakati huo huo, shahidi mwingine, Bw Lewis Thoya, aliambia mahakama jinsi nduguye, Evans Kolombe Sirya, alivyoacha biashara yake yenye faida tele na kujiunga na kanisa la Mackenzie huko Malindi kabla ya kuhamia msituni.
“Ndugu yangu alikuwa amefanikiwa sana katika biashara yake na alikuwa akinisaidia sana kwani alikuwa akipata pesa nyingi kutokana na biashara yake. Alifanya kazi kama mwanakandarasi katika mji wa Malindi,” alieleza.
Bw Thoya alisema kuwa, mambo yalibadilika wakati Kolombe alipowaondoa watoto wake shuleni kule Malindi mnamo 2018 baada ya kuwa muumini wa kanisa la Mackenzie huko Furunzi.
Alisimulia kuwa licha ya juhudi za kumsihi Kolombe kuwarudisha watoto shuleni wakati wa mkutano wa familia, maombi yake hayakuzaa matunda.
“Nilimwalika kaka yangu nyumbani kwangu na kumhoji kuhusu uamuzi wake, ambapo alijibu kuwa elimu ni kinyume na mapenzi ya Mungu. Pia alisema kuwa watoto wake hawatapata elimu rasmi,” Bw Thoya alisema.
Familia hiyo hatimaye ilihamia msituni. Bw Thoya alisema kakake alikuwa na watoto sita na kuongeza kuwa alimuona Kolombe mara ya mwisho mwaka wa 2018 baada ya kujiunga na kanisa la Mackenzie.
Alisema kuwa, kakake alikuwa mtu mwenye bidii na makini, kuanzia wakati wake katika shule ya upili na chuo kikuu kabla ya kujiunga na kanisa la Mackenzie.