Habari za Kitaifa

Mutua ataka Kalonzo aheshimiwe washirika wa Ruto wakitofautiana Ukambani

Na KITAVI MUTUA, PIUS MAUNDU January 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Leba Dkt Alfred Mutua amewataka viongozi na maafisa wa serikali kutoka eneo la Ukambani kumheshimu kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, huku washirika wa Rais William Ruto eneo hilo wakitofautiana vikali.

Badala ya dharau na majibizano ya kisiasa kama ilivyotazamiwa, Dkt Mutua alishangaza mkutano wa viongozi wa Ukambani mnamo Ijumaa alipotoa wito huo wa heshima kwa Bw Musyoka ambaye anaungwa mkono na wakazi wengi kutoka Ukambani.

“Nataka sote tumpe Kalonzo Musyoka heshima anayostahili. Viongozi wote lazima waheshimiwe kama hatua ya kwanza ya kufikia umoja wa kisiasa ambao kila mtu katika jamii anatamani,” Waziri alisema.

Alisema ndoto yake ni kuona viongozi wa Ukambani wameacha misimamo ya vyama na kuungana ili kujadili changamoto zinazokumba wakazi wa eneo hilo.

“Natamani kuwepo mkutano unaoleta pamoja Bw Musyoka, Johnson Muthama na viongozi wengine wakuu Ukambani, na tuzungumze kwa sauti moja,” alieleza.

Hata hivyo, ndoto yake ilipata pigo hata kabla kuanza kuchomoza kwani hakuna kiongozi yeyote aliyechaguliwa kupitia tikiti ya Wiper alifika kwa mkutano wa mashauriano alioitisha katika hoteli ya Maanzoni.

Isitoshe, washirika wa kisiasa wa Dkt Mutua ndani ya muungano tawala wa Kenya Kwanza pia walisusia. Waziri huyo alihubiri amani na upendo hata kwa wakinzani wao, akihimiza 2025 uwe mwaka wa kukumbatia wapinzani ili kufanikisha umoja wa jamii ya Kamba.

Mkutano huo wa mashauriano uliishia kuanika tofauti kali ambazo zimetikisa washirika wa Rais Ruto katika eneo la Ukambani.

Washirika wa Rais wanaohusishwa na Dkt Mutua wametofautiana na wabunge watatu waliochaguliwa kwa tikiti ya vyama vya muungano wa Kenya Kwanza eneo hilo.

“Kwa sababu ni wazi anang’ang’ania kuwa msemaji wa Rais Ruto eneo la Ukambani, Dkt Mutua kwanza ana kibarua cha kumvumisha rais Ukambani jinsi tumekuwa tukifanya kwa miaka mingi,” alitanguliza Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka.

“Njia bora ya kuvutia watu wamuunge Rais Ruto ni kutekeleza majukumu yetu kikamilifu. Dkt Mutua kwanza awajibike kwa wizara anayoongoza,” Bw Musyoka aliambia Taifa Jumapili kwenye mahojiano jana.

Mbunge huyo, ambaye ni Kaimu Katibu Mratibu wa chama tawala cha UDA, alikuwa akijibu dai la Dkt Mutua kuwa kiunganishi cha Rais Ruto na eneo la Ukambani eti kwa sababu ndiye kiongozi wa Ukambani aliye na wadhifa wa juu serikalini.

Wito huo wa heshima na umoja wa Ukambani ulishamiri kongamano lililoleta pamoja baadhi ya wanasiasa na wataalamu kutoka eneo hilo, liloandaliwa katika hoteli ya Machakos mnamo Ijumaa.

Huku waliozungumza wakikemea ukosefu wa maendeleo katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni, Dkt Mutua alikita kupigia debe maendeleo ya Rais Ruto kama vile nyumba za bei nafuu na huduma ya afya kwa wote.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA