Habari za Kitaifa

Muturi alitabiri masaibu ya Gavana Mwangaza

Na CHARLES WANYORO August 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA Kawira Mwangaza alipokuwa akizindua kampeni ya kuwania kiti cha Meru mnamo Machi 2022, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alisisitiza umuhimu wa kuwa na madiwani waaminifu kwake.

Ni kama alidadisi kilichokuwa kikimsubiri huku akimuonya Bi Mwangaza kuwa angekabiliwa na vitisho vya kutimuliwa iwapo asingekuwa na madiwani wa kutosha upande wake katika Bunge la Meru.

Huku akimrai kujiunga na chama cha DP, Bw Muturi alitabiri Bi Mwangaza angekabiliwa na hali ngumu iwapo angewania kama mgombeaji huru.

“Gavana lazima awe na madiwani wa kutosha walio upande wake katika Bunge. Kama unavyojua, kila mtu akiwa huru kuna hatari ya kuhujumiwa,” Bw Muturi alitahadharisha wakati huo.

“Tumeona jinsi madiwani wanavyosumbua magavana baada ya kuchochewa kisiasa, nataka kuwasihi, mpeni madiwani ambao hawatamhujumu. Hatungependa hali ambapo atawekwa afisini kisha madiwani wengine washirika wa vyama vingine wakose kumpa nafasi ya kuhudumia watu wake.”

Bw Muturi ambaye kwa sasa ni Waziri wa Utumishi wa Umma, amegeuka kuwa nabii wa kweli huku aliyosema yakitimia.

“Atakuwa akiamka kukabiliana na vitisho vya kuondolewa mamlakani ili akubali matakwa mbalimbali. Msikubali ashindwe, mpeni watu wenye mapenzi mema, watu wanaoamini katika utoaji wa huduma kwa mwananchi ili asikose kushughulikia maendeleo kwa kukabiliwa na upinzani,” aliwasihi wafuasi wake.

Miaka miwili baadaye, Bi Mwangaza yuko kortini akipinga kuondolewa kwake ambako kuliidhinishwa na Seneti mnamo Agosti 20, 2024.

Na kama Bw Muturi alivyodokeza, mwakilishi wa wadi ya Meru aliyekuwa shahidi wa Bi Mwangaza alifichua kuwa madiwani katika kaunti hiyo walihimizwa na chama kuunga mkono hoja za kuondolewa madarakani gavana huyo.

Aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Meru, Bw Evans Mawira ambaye aliwasilisha hoja ya pili ya kumtimua Bi Mwangaza alisema uongozi wa UDA ulitaka madiwani wote 21 wa chama hicho kuunga mkono kuondolewa ofisini kwa gavana huyo.