Habari za Kitaifa

Muturi: Mawaziri siku hizi hawashiki simu yangu, wanaogopa Ruto

Na CHARLES WASONGA April 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Waziiri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi amefichua kuwa Rais William Ruto huwatia woga mawaziri wake kiasi kwamba hawawezi kusemezana waziwazi wala kukosoa baadhi ya maamuzi mabaya ya serikali.

Kwenye mahojiano na runinga ya NTV Ijumaa asubuhi, Aprili 4, 2025, Bw Muturi aliongeza kuwa tangu alipoanza kuikashifu serikali kuhusiana na suala la utekaji nyara, na hatimaye akafutwa, mawaziri hao wamedinda kujibu simu zake, zikiwemo jumbe za WhatsApp.

Alidai mawaziri hao wanaogopa huenda wakaadhibiwa ikigunduliwa kwamba waliongea naye.

“Badala yake, baadhi yao sasa huniomba nitumie laini nyingine ya simu au watu wengine wawapigie kwa niaba yangu ili isibainike kuwa walizungumza nami. Wanaogopa kwamba mawasiliano yao nami yatanaswa, hali ambayo itawaweka pabaya na bosi wao,” Bw Muturi akaeleza.

Aidha, Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani alidai kuwa mawaziri hao huwa hawahoji kauli au maamuzi ya Rais Ruto katika mikutano ya baraza la mawaziri kwa sababu wanamwogopa.

“Zamani kwa hakikika mawaziri walikuwa huru kuchangia mawazo yao kuhusu masuala mbalimbali wakiwa katika kamati ndogo zilizoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na sasa Profesa Kithure Kindiki,” Bw Muturi akaeleza.

Alieleza kuwa katika vikao vya baraza la mawaziri chini ya uongozi wake, Dkt Ruto hutaka kauli zake zizingatiwe wakati wa utekelezaji miradi ya mabilioni ya fedha katika wizara mbalimbali.

Wakati huohuo, Bw Muturi alifuchua kuwa bwanyenye Narendra Raval, almaarufu Guru ni mwandani wa karibu wa Rais Ruto na hufaidi kutokana na miradi mikubwa ya serikali.

Guru ni mmiliki na mwenyekiti wa Kampuni ya Devki iliyowekeza katika sekta za utengenezaji vyuma, saruji na vifaa vingine vya ujenzi.