Habari za Kitaifa

Mutuse alivyotolewa jasho na mawakili wa Gachagua katika Seneti

Na DANIEL OGETTA, BENSON MATHEKA October 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ILIKUWA jioni ngumu kwa Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse alipohojiwa vikali na mawakili wa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika Seneti.

Mawakili wa Gachagua, akiwemo Elisha Ongoya na Tom Macharia, walimkosoa mbunge huyo kuhusu hoja yake ya kuondolewa mamlakani kwa Naibu Rais wakitaka kutia doa madai aliyotoa Bungeni.

Mbunge huyo mara nyingi alijipata akijitetea huku akihojiwa vikali kutokana na hoja yake ya kumuondoa Bw Gachagua mamlakani.

Bw Mutuse kwanza alieleza maseneta misingi ya hoja yake, akisema naibu rais alikuwa amekiuka vipengee mbalimbali vya Katiba.

“Kwa miaka miwili iliyopita, Naibu Rais ametembelea maeneo mbalimbali nchini Kenya na amekuwa akitangaza kwamba Kenya ni kampuni inayomilikiwa na wenyehisa na kwamba wanaomiliki hisa katika kampuni hiyo iitwayo Kenya wangenufaika kimaendeleo katika masuala ya huduma. Tunasema kwamba Kenya si kampuni,” alisema.

Baada ya Mbunge huyo kuhutubia maseneta, wakili Ongoya alipanda jukwaani kupinga mashtaka mbalimbali dhidi ya Naibu Rais, akianza na madai kwamba Bw Gachagua alimtishia Jaji Esther Maina wa Mahakama Kuu. Hapo awali, Jaji Maina alikuwa ameamua kwamba Bw Gachagua, ambaye wakati huo alikuwa mbunge, alikosa kueleza jinsi alivyopata utajiri kutoka mashirika ya serikali.

Wakili Ongoya alikosoa madai ya Mbunge Mutuse kuhusu Bw Gachagua na Jaji Esther Maina.

Uchunguzi huo pia uligusia madai ya Bw Mutuse kwamba Gachagua alitumia kampuni zake kujitajirisha kupitia ufisadi.

Mbunge Ongoya pia alimhoji Bw Mutuse kuhusu sehemu za hoja yake zinazogusa matamshi ya Gachagua wakati wa ubomoaji wa Kayole.

Wakili Ongoya apingana na Mbunge Mutuse kuhusu matamshi ya DP Gachagua wakati wa ubomoaji Kayole

“Je, Baraza la Mawaziri liliidhinisha azimio la kutoshirikisha hisia za wananchi katika ubomoaji?” alimuuliza mbunge huyo.

“Siwezi kujua kwa sababu siko katika Baraza la Mawaziri,” mbunge huyo alijibu.

“Na bado unasema kuwa wito wa Naibu Rais kuwashirikisha wananchi ni sehemu ya ukiukaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri?”

“Katika muktadha,” Mbunge Mutuse alisema.

“Nataka kujua: watu waliokuchagua, wataheshimu tabia hii hapa?”

“Mheshimiwa Spika naomba ulinzi wako. Watu wa Kibwezi hawako kwenye kesi.”

Akimhoji Mutuse, Bw Macharia alicheza video ikimuonyesha Rais William Ruto akihutubia umati mjini Murang’a. Katika kanda hiyo, Dkt Ruto anakiri kuwateua watu kutoka eneo hilo katika nyadhifa kuu za serikali, akiwataja kama “wenyehisa” katika utawala wake.

“Nani alikuwa anaongea kwenye hiyo video?” wakili aliuliza.

“Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto,” akajibu Bw Mutuse.

Bw Macharia aliendelea, akiuliza ikiwa kweli Rais alikuwa amewataja wakazi wa Murang’a kama “wenyehisa wakuu” wa serikali. Mutuse alithibitisha, akisema, “Ndiyo, alikubali.”

Wakili huyo kisha alishangaa jinsi Bw Mutuse anavyoweza kumkashifu naibu rais kwa kuunga mkono maoni ya Rais.

“Wakati naibu rais anamsaidia Rais katika kujadili wenyehisa, je, hilo linakuwaje kosa lisiloweza kuepukika?” Bw Macharia aliuliza.

Bw Mutuse alishikilia kuwa lugha kama hiyo haikupewa Rais kikatiba, na pia haikufaa kwa naibu rais kuitumia.