Mwanaharakati Bonface Mwangi akamatwa na polisi, mkewe asema
Mwanaharakati Boniface Mwangi, ameripotiwa kukamatwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Kwa mujibu wa mkewe Njeri Mwangi na wanaharakati wenzake, Mwangi alikamatwa Jumamosi mchana nyumbani kwake katika eneo la Lukenya, Kaunti Ndogo ya Mavoko, Kaunti ya Machakos.
Alifichua kuwa mara baada ya kukamatwa, maafisa hao walichukua simu za Mwangi na wakasema wanampeleka katika makao makuu ya DCI yaliyoko Barabara ya Kiambu, Nairobi.
“Polisi wamefika nyumbani kwetu Courage Base na wanamchukua mume wangu, wakizungumza kuhusu ugaidi na uchomaji moto! Wamechukua vifaa vyake na kusema wanampeleka makao makuu ya DCI. Siwezi kupumua,” alisema mkewe.
Boniface Mwangi amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais William Ruto, akiilaumu kwa kupanga utekaji nyara na mauaji ya kiholela. Hivi karibuni alikashifu serikali kwa kutochukua hatua licha ya yeye kutiwa mbaroni na kuteswa nchini Tanzania.
Kukamatwa kwake kunajiri siku moja baada ya kuwasilisha kesi dhidi ya serikali ya Rais Samia Suluhu wa Tanzania katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
Katika kesi hiyo iliyowasilishwa Ijumaa, Julai 18, na Mwangi, Agather Atuhaire na mashirika saba ya kijamii, serikali ya Tanzania inatuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Ukiukaji huo unajumuisha kutoweka kwa kulazimishwa, mateso, kuwekwa kizuizini kiholela, unyanyasaji wa kijinsia, na kufukuzwa nchini kinyume cha sheria.
Wanaharakati hao pia wanataka serikali za Tanzania, Kenya na Uganda ziombe msamaha rasmi, na pia kulipwa fidia ya Sh130 milioni kila mmoja.
Kukamatwa kwa Mwangi kulithibitishwa na Hussein Khalid, Mkurugenzi Mtendaji wa Vocal Africa, aliyesema alikuwa na mawakili kufuatilia suala hilo.
“Nathibitisha kuwa Boniface Mwangi amekamatwa nyumbani kwake Courage Base na maafisa kutoka DCI. Pamoja na mawakili wake, tunafuatilia ili kujua sababu ya kukamatwa kwake,” alisema Khalid.
Ingawa polisi bado hawakuwa wametoa taarifa rasmi kuhusu kukamatwa wakati wa kuchapisha ripoti hii, ripoti zinaeleza kuwa anachunguzwa kuhusiana na madai ya kuhusika katika maandamano ya hivi majuzi jijini Nairobi na miji mingine, ambapo mali iliharibiwa na kuporwa.
Zaidi ya watu 1,000, wengi wao wakiwa vijana, wamekamatwa kuhusiana na maandamano hayo, huku baadhi tayari wakifikishwa mahakamani kwa mashtaka mbalimbali.
Maandamano ya hivi majuzi yaligeuka kuwa ya vurugu, ambapo mashirika ya haki za binadamu yanakadiria kuwa takriban watu 50 waliuawa katika makabiliano na maafisa wa usalama.