Mwanariadha aliyekufa maji akiokoa mbwa wa mwajiri Mexico azikwa
VITALIS KIMUTAI NA LABAAN SHABAAN
FAMILIA na marafiki walimuaga miaka 17 iliyopita akisafiri kuenda Nairobi kuabiri ndege kuelekea Amerika Kusini kushiriki mbio kadhaa alizoratibiwa.
Kama ilivyokuwa desturi, walimtarajia arudi Kenya baada ya miezi sita ya mashindano ya riadha nchini Mexico – ambapo alitafutia familia yake riziki kutumia talanta yake.
Josephat Kibet Ngetich, hata hivyo, amerejea kuungana na familia yake na kupokewa, si kwa nderemo, bali kwa huzuni na vilio mwili wake ukiwa ndani ya jeneza.
Alipokewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na kijijini Taabet eneo bunge la Bomet ya Kati, kaunti ya Bomet.
Soma pia Mwanariadha Kiptum alivyochangamsha watu Monaco akihutubu kwa Kiswahili
Ngetich, baba wa watoto watatu, alifariki nchini Mexico alipokuwa akijaribu kumwokoa mbwa aliyeanguka ndani ya bwawa katika shamba la mwajiri wake mnamo Desemba 14, 2023.
Haijawekwa bayana ikiwa mbwa huyo alinusurika kisa hicho au pia alikufa.
Jozi ya viatu vya michezo alivyokuwa akivitumia katika mbio mbalimbali vilikuwa juu ya jeneza wakati lilikuwa linatolewa kutoka chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Longisa Ijumaa jioni.
Maiti hiyo ilipelekewa huko juma moja lililopita kwa maandalizi ya mazishi.
“Tunaishukuru serikali ya kitaifa kupitia idara ya Mashauri ya Kigeni, Ubalozi wa Mexico nchini Kenya, viongozi wa eneo hili wakiongozwa na Mbunge wa Bomet ya Kati Richard Kilel, wanahabari, marafiki, jamaa na waliotufaa kwa msaada na maombi kwa miezi miwili iliyopita,” Bi Janeth Ngetich, mjane alisema wakati wa mazishi Jumamosi.
Soma pia Majonzi nyota wa rekodi ya dunia ya marathon, Kiptum akiaga dunia
Kwa muda wa miezi miwili, familia hiyo imekuwa na majonzi na wasiwasi kama mwili wa marehemu ungesafirishwa hadi Kenya kwa mazishi.
Ni kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kukusanya Sh3 milioni walizokuwa wakihitaji kutokana na hali ya uchochole.
Lakini serikali za Kenya na Mexico ziliingilia kati na kuwezesha mwili huo kurudishwa nyumbani, bila gharama yoyote kwa familia.
“Imekuwa miezi miwili ya kutokuwa na uhakika. Serikali imesaidia sana familia na kamati ya mipango ya mazishi. Tuna furaha kukamilisha mipango hii,” alisema Bw Paul Ngetich ambaye alishirikisha timu ya Kenya ya kusimamia mipango ya mazishi.
Bw Geoffrey Kirui, mwanariadha wa Kenya nchini Mexico ambaye anatoka eneo bunge la Bomet Mashariki, aliongoza timu ya dayaspora kuratibu mchakato wa kumrejesha nyumbani marehemu.
Soma pia Wakenya wanaotumia X wamshambulia mwanariadha Kipchoge kwa rambirambi zake kwa Kiptum
Kulikuwa na ukosefu wa stakabadhi sahihi za marehemu zilizochelewesha mpango huo na masharti magumu yaliyotolewa na idara ya polisi nchini Mexico.
“Tuna furaha kuwa Ngetich amezikwa baada ya shughuli ngumu ya kurudisha mwili wake Kenya kwa ibada ya mwisho na familia ya karibu,” Bw Kirui aliambia Taifa Leo kutoka Mexico Jumapili.
Mnamo Januari 15, Seneta Maalum Joyce Korir alimwarifu Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu masaibu ya familia.
Huu ulikuwa wakati Naibu Rais alihudhuria mazishi ya marehemu Philip Kipsigei Langat Tonui, babake Seneta wa Bomet Hillary Sigei, katika kijiji cha Kapsiyo, eneo bunge la Chepalungu.
Kilio hiki kilisababisha ufuatiliaji wa haraka wa mchakato wa kurudisha mwili nyumbani kwa ushirikiano na Wakenya nchini Mexico.
Soma pia Ubabe uliotarajiwa kati ya Kiptum na Kipchoge katika 42km wazimwa na kifo cha ghafla
Ndege iliyobeba mwili huo ilitua JKIA saa tatu na nusu usiku mnamo Februari 9, Taifa Leo ilibaini kupitia stakabadhi za usafiri.
Marehemu alisafirishwa kupitia ndege ya British Airways iliyoondoka Mexico Februari 7 na kusimama Uingereza kabla ya kutua JKIA Nairobi siku mbili baadaye.
“Ni kipindi cha huzuni kwetu kumpokea mwanangu kwenye jeneza baada ya miaka yote aliyokuwa nje ya nchi. Lakini tunashukuru kwamba kwa usaidizi ambao tumepokea, tunaweza kumzika kwa heshima na kufunga suala hili,” Bi Pauline Nowa, mamake marehemu alisema.
Bi Nowa alifichua kwamba aliuza kipande cha ardhi ya familia ili kupata tikiti ya ndege na kumtunza mwanawe akiwa ughaibuni.
Alikuwa na matumaini kuwa mwanariadha huyo angebadilisha maisha ya familia yao.
Lakini masaibu yaliibuka mwaka wa 2006 Ngetich alipopata jeraha la goti ambalo halikupona kumwezesha kushiriki tena mashindano ya riadha.
Inasemekana alipoteza hati zake za usafiri na hakuweza kujisajili tena.
Hali hii ilimfungia Mexico ambapo alifanya kazi za mikono ili kujimudu alipofanya kazi za kijungu jiko na ujakazi shambani.
Kulingana na rekodi za Shirikisho la Riadha Duniani, Ngetich alishiriki katika mbio kadhaa zilizorekodiwa Amerika Kusini (Mexico).
Mbio hizo zilihusisha zile za mita 3,000 kuruka viunzi na maji ambazo Wakenya wametawala kwa miaka mingi kwenye jukwaa la kimataifa.