Habari za Kitaifa

Mzozo wa ndani kwa ndani unavyotishia kusambaratisha ndoto ya Raila AUC

Na JUSTUS OCHIENG November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MASWALI yameibuika kuhusu ziliko pesa za kugharimia kampeni za Kinara wa Upinzani Raila Odinga huku mzozo wa ndani kwa ndani ukitishia kusambaratisha azma yake ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Mnamo wikendi, ilibainika kuwa wanachama 10 wa sekretariati inayoongoza kampeni za Bw Odinga haijalipwa hata shilingi licha ya serikali kutoa pesa hizo jinsi alivyoahidi Rais William Ruto.

Sekretariati ya Raila ina wanachama kutoka Afisi ya Rais (ikulu), Wizara ya Masuala ya Kigeni na pia wapangaji mikakati na wataalamu ambao waliteuliwa na Raila mwenyewe.

Alipowaongaza marais wa ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuzindua azma ya Raila mnamo Agosti 27, Rais William Ruto alihakikishia nchi kuwa kampeni za Raila zitagharimiwa na serikali.

Hakikisho kama hilo lilitolewa na Kinara wa mawaziri Musalia Mudavadi ambaye amekuwa akisawiri Raila kama mwaniaji wa serikali na hata wikendi aliandamana naye alipozindua azma yake jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Taifa Leo iliarifiwa kuwa, mgao wa kugharimia kampeni za Raila ulikuwa umeidhinishwa na Baraza la Mawaziri na hadi leo, ni kitendawili mahali ambapo hela hizo zimekuwa zikielekezwa.

Pesa hizo zilijumuishwa kwenye bajeti ambayo iliandaliwa mwaka huu japo hazijafichuliwa hadi sasa ni pesa ngapi.

Jana, mwanachama wa sekretariati hiyo alilalamikia njaa ambayo ipo katika kambi yao huku akisema hawajalipwa hata shilingi ilhali wamekuwa wakiwajibika kuhakikisha Raila anatamba kwenye siasa za Afrika.

“Mshahara wetu kwa mujibu wa bajeti ambayo iliandaliwa Juni ni Sh40,000 kwa kila mmoja wetu kila mwezi. Tuko 10 pamoja na wafanyakazi wawili,” akasema mwanachama wa sekretariati ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.

“Kumbuka pia kuwa kuna Wizara ya Masuala ya Kigeni, wafanyakazi wa afisi ya Rais lakini hao wanalipwa mshahara na waajiri wao,” akaongeza.

Aliyekuwa Balozi wa Kenya kule Amerika Elkana Odembo ambaye ni mwenyekiti wa sekretariati ya Raila alionekana kulemewa na suala la fedha zaidi huku madai yakizuka kati ya wanachama kuwa wanasiasa wamekuwa wakifadhiliwa ilhali wao hawajalipwa.

Pia kumezuka madai kuwa chombo cha usalama cha serikali sasa kimetwaa kazi ya sekretariati hiyo na ndiyo sasa inasimamia kampeni za Raila.

“Kwa sasa mambo si mazuri jinsi ambavyo watu hapa nje wanavyofikiria. Tunahofia kuwa mgao ni mkubwa na tayari ushatolewa lakini haujatufikia. Kampeni zikiisha tutajitetea kivipi iwapo kutakuwa na madai ya kiasi kikubwa kutolewa ilhali sisi hatukunufaika?”

Mnamo Jumapili, Bw Odembo alikataa kugusia suala la mahali ambapo pesa za Raila zilielekezwa, akisema wanamakinikia kampeni zake zifaulu.

Licha ya sekretariati kutopata pesa, lawama zimetanda kuwa wanasiasa wamekuwa wakigharimiwa safari zao kila mara Raila akiwa kwenye kampeni huku wanachama wa sekretariati wakiachwa nje.

Akiwa Addis Ababa Ijumaa na Jumamosi, Raila aliandamana na wanasiasa wengi wakuu wa ODM ambao walihudhuria hafla ya uzinduzi wake.

“Tuliambiwa kuwa walisafiri kwa kuketi sehemu ya abiria wa hadhi kwenye ndege na kuishi katika hoteli za kifahari ilhali wanachama wa sekretariati hawajalipwa pesa zao,” akaongeza mwanachama huyo wa sekretariati.

Bw Odembo hata hivyo alikanusha kuwa sekretariati ndiyo iliwalipia wanasiasa hao gharama ya usafiri na hoteli wakiwa Ethiopia.

“Mwanasiasa mmoja pekee aliyeniambia alikuwa akija ni Walter Owino (Mbunge wa Awendo). Wengine walitaka waje bila Raila kujua na kwa kweli hata naye alishangaa na kufurahia uwepo wao,” akasema Bw Odembo.

Kati ya wanasiasa ambao walifika Addis kwa hafla ya Raila ni Naibu Kiongozi wa ODM Geodfery Osotsi, Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, wabunge Junet Mohamed (Suna Mashariki), Rozah Buyu (Kisumu Magharibi) na Ruth Odinga (Kisumu).

Pia maseneta Aaron Cheruiyot (Kericho), Tom Ojienda (Kisumu) na Naibu Gavana wa Siaya William Oduol walikwepo.

Bado kuhusu pesa, kuna makundi ambayo yameanza kuzuka kwenye sekretariati ambayo yanaotea pesa zikizisubiri na pia zinataka kudhibiti kampeni za Raila.