Habari za Kitaifa

Natembeya ‘alikopa’ Sh9 milioni za wagonjwa kushiriki kongamano la ugatuzi 2023, Mkaguzi wa Fedha afichua

Na MARY WANGARI April 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kaunti ya Trans Nzoia, George Natembeya, amemulikwa kwa kutumia mamilioni ya pesa zilizokusanywa kutoka kwa wagonjwa kufadhili serikali yake kushiriki kongamano la ugatuzi 2023.

Kongamano la Ugatuzi 2023 lilifanyika katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, ilifichua jinsi Sh9.45 milioni zilitolewa kutoka akaunti ya Hospitali ya Rufaa ya Kitale wakati ambapo taasisi hiyo ya afya inakabiliwa na ukosefu wa vifaa muhimu.

Hospitali hiyo ya Level 4 haina vitanda vya Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na HDU wala wataalamu wanaohitajika katika matibabu ya upasuaji huku ikiwa na maafisa 14 wa matibabu, mkaguzi mkuu alifichua katika ripoti ya mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2024.

Hii ni kinyume cha sheria inayohitaji hospitali ya Level 4 kuwa na vitanda sita vya ICU na sita vya HDU, ikiwemo wataalamu wawili wa upasuaji na maafisa 16 wa matibabu.

Isitoshe, Kamati ya Seneti kuhusu Matumizi ya Fedha za Serikali ilisikia katika kikao Jumanne, Aprili 1, 2025 kwamba Hospitali ya serikali ya kaunti ilitoa fedha hizo pasipo idhini kutoka kwa bodi ya Hospitali.

Aidha, hakukuwa na stakabadhi zozote kuonyesha mkataba kati ya serikali ya kaunti na usimamizi wa serikali.

Gavana Natembeya akijibu maswali mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Vihiga, Godfrey Osotsi, alisema alikopa hospitali fedha hizo kwa sababu hazina kuu ilichelewesha kutoa mgao wa kaunti.

Alikiri fedha hizo zilitumika kufadhili idara mbalimbali za usimamizi wake kuhudhuria kongamano hilo.

“Tumekubali ukopaji huo. Ilifanyika hivyo kwa sababu hatukuwa na bajeti ya kongamano la ugatuzi hivyo basi tukakopa ili kushiriki kongamano,” alieleza Gavana Natembeya.

Mkuu huyo wa kaunti alihakikishia Seneti kwamba “tutahakikisha fedha hizo zinarejeshwa katika bajeti hii, kabla ya mwaka kuisha.”

Huku akisema ukopaji huo uliendeshwa na maafisa wakuu katika idara za afya na fedha, Gavana alishindwa kutoa ushahidi kuonyesha maafikiano au idhini ya hatua hiyo.

Seneta wa Trans Nzoia Allan Chesang aliuliza “kazi ya bodi ya hospitali ni gani ikiwa idhini inaweza kutolewa ndani kwa ndani, pesa zitolewe na zitumike pasipo mchango wa bodi?”

“Hata ikiwa ni ukopaji wa ndani kwa ndani, bodi ya hospitali inahitaji kuidhinisha? Sheria inaruhusu aina hiyo ya kukopa wazi? kunahitajika idhini kutoka kwa bodi ya hospitali?” alihoji Seneta Mteule Peris Tobiko.

Kifungu 142 cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma 2012 kinasema “bunge la kaunti linaweza kuidhinisha ukopaji wa muda mfupi kutoka kwa taasisi za serikali za kaunti kwa shughuli za pesa taslimu pekee.”

Kiasi cha pesa kinachokopwa hakipaswi kupita asilimia tano ya mapato yaliyokaguliwa majuzi ya taasisi husika ambayo inapaswa vilevile kuhakikisha fedha zilizokopwa zinalipwa katika muda usiozidi mwaka mmoja kutoka tarehe ambayo zilikopwa.

“Mbona inachukua muda mrefu kurejesha hela ilhali sheria inasema wazi pesa hizo zinapaswa kulipwa?” Aliuliza Seneta Osotsi.

Ripoti hiyo ilielezea wasiwasi kwamba hali duni ya hospitali hiyo ya kaunti inakiuka haki za wakazi kuambatana na Kifungu 43(1)(a) cha Katiba kuhusu kupata huduma bora za afya, ikiwemo zinazohusu afya ya uzazi.

Mkaguzi Mkuu vilevile alizua maswali kuhusu zilipokwenda Sh3 milioni zilizopokewa kutoka kwa wahisani na washiriki wa maendeleo huku usimamizi wa hospitali ukishindwa kuwasilisha nakala za muafaka na wafadhili wake.