Ni kuoga na kurudi soko: Linturi alenga ugavana baada ya kufukuzwa serikalini
ALIYEKUWA Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi, sasa ameelekeza macho yake kwa kiti cha ugavana Meru akisema hatua ya kumtimua serikalini huenda ilikuwa baraka.
Bw Linturi, alikwenda mafichoni baada ya kufurushwa kutoka baraza la mawaziri na kujitokeza kwa mara ya kwanza hadharani Septemba 1 akiandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Waziri huyo wa zamani aliwania kiti cha ugavana Meru 2022 na kuibuka wa pili akijitwalia kura 183,859 dhidi ya kura alizozoa Gavana Kawira Mwangaza, 209,148.
Siku chache zilizopita, Bw Linturi alitangaza kuwa ameanza kampeni yake kuwa mkuu wa Kaunti ya Meru 2027.
Yupo mbioni kufufua mahusiano yake kisiasa na wanasiasa kadhaa maarufu akiwemo mbunge wa zamani Igembe Kaskazini Maore Maoka na madiwani wa zamani huku akijiandaa kuwabwaga washindani wake.
Kwa sasa, Bw Linturi amekuwa akizuru maeneo mbalimbali nchini akikosoa utawala uliopo.
“Macho yangu yamelenga shabaha. Ikiwa yeyote anafikiri sitashinda kiti cha ugavana Meru 2027, wanaota. Nawasihi wote walionipigia kura 2022 kuhifadhi vyema kura zao na waniruhusu niziongeze. Ninakuja kurekebisha serikali ya kaunti ya Meru sawa na nilivyolainisha wizara ya kilimo,” alisema.
Bw Linturi, aliyetawazwa kuwa msemaji wa Njuri Ncheke kabla ya kung’atuliwa, alisema hana hamu tena na teuzi ambapo mamlaka inayoteua inaweza kupiga kalamu kwa hiari.
“Nachukulia kutimuliwa kwangu kutoka baraza la mwaziri kuwa baraka fiche. Hii ni kwa sababu kutanipa muda wa kutosha kusaka kura. Mwaka 2022, nilijiunga na kinyang’anyiro miezi mitatu kabla ya uchaguzi na nikawa nambari mbili. Sasa nina miaka mitatu ya kujiandaa. Kwa kila wingu kuna heri,” alisema Bw Linturi.
Seneta huyo wa zamani anamchukulia aliyekuwa gavana Peter Munya kama anayeweza kuwa na ushindani mkali katika chaguzi za 2027.
Kando na kumsuta Bi Mwangaza kwa madai ya kusambaratisha kaunti, Linturi alisema Munya anafaa kulaumiwa kwa kumuunga mikono Mwangaza 2022.
“Tatizo tulilo nalo Meru linaweza kuelekezwa kwa Bw Munya kwa sababu nilipogombea 2022, aliunga mkono mpinzani wangu. Kwa sababu ndiye kiini cha masaibu tuliyo nayo, hafai kuyaponya,” alisema.