• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
Mithika Linturi ateua mgombeaji mwenza

Mithika Linturi ateua mgombeaji mwenza

NA GITONGA MARETE

SENETA wa Meru Mithika Linturi ameteua wakili mwanamke kuwa mgombea mwenza wake katika maandalizi ya kushindana na Gavana Kiraitu Murungi na Mwakilishi wa Kike Kawira Mwangaza.

Seneta huyo anagombea ugavana kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto huku Bw Murungi akitetea kiti chake kwa tikiti ya chama chake cha Devolution Empowerment Party (DEP).

Bi Mwangaza atamenyana na wanaume hao akiwa mgombea huru.

Kwa kumteua Bi Linda Kiome, wakili wa Mahakama Kuu aliye ya umri wa chini ya miaka 40 kuwa mgombea mwenza wake, Bw Linturi analenga kuwavutia wanawake na vijana ambao alisema wamekuwa wakipuuzwa katika uongozi wa kaunti hiyo.

“Nilisikitika wakati bunge la sasa lilikosa kuweka sheria ya kuhakikisha usawa wa jinsia. Lakini baadhi ya mambo kama haya sio lazima yawe katika sheria zetu ili yatekelezwe. Yanahitaji uwajibikaji wetu na kutambua kwamba wanawake ambao ni nusu ya idadi yetu wanafaa kuhusishwa katika uongozi katika viwango vyote,” alisema Bw Linturi.

Seneta huyo alitangaza Bi Kiome kuwa mgombea mwenza wake katika Alba Hotel mjini Meru Jumapili usiku katika sherehe iliyohudhuriwa na wabunge Kubai Kiringo (Igembe ya Kati) na Kathuri Murungi (Imenti Kusini) na wawaniaji kadhaa wa ubunge na udiwani.

Bw Kathuri anagombea useneta kaunti ya Meru kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kwa tikiti ya UDA.

Bw Linturi alisema kabla ya kuamua kumteua Bi Kiome, alizungumza na watu kadhaa akifanya utafiti na majadiliano na baada ya kuchagua wawili kutoka orodha ya watu 12, walihojiwa na jopo la wataalamu saba.

“Ulikuwa mchakato wenye mashauriano na kwa miezi miwili, tulizungumza na wakazi na pia tufanya kura ya maoni ambayo wapigakura zaidi ya 78, 000 waliniambia kwamba walitaka naibu gavana mwanamke anayewakilisha vijana. Sina nguvu za kuwanyima haki yao,” alisema.

Bi Kiome alishukuru kwa uteuzi huo akiutaja kama “ushahidi wa kutambuliwa kwa jukumu la vijana na wanawake katika siasa” na akaahidi kurai vijana kumchagua Bw Linturi kama gavana wa tatu wa Meru.

Hueda kiti cha ugavana kaunti ya Meru kikachukuliwa na mgombeaji atakayefaulu kushawishi koo tatu za Imenti, Igembe na Tigania.

Akiwa na mgombea mwenza kutoka Imenti Kaskazini na Bw Kathuri upande wake, Bw Linturi anayetoka Igembe Kusini anasema amejipanga kumshinda Bw Murungi.

Bw Linturi pia anategemea uungwaji mkono na wabunge wanane kati ya 11 wa kaunti ya Meru walio katika UDA.

Wabunge hao ni John Paul Mwirigi (Igembe Kusini), Kirima Ngucine (Imenti ya Kati), Mugambi Rindikiri (Buuri), Bw Kiringo, Bw Kathuri, Gichunge Kabeabea (Tigania Mashariki), Halima Mucheke (Maalum, ambaye sasa anagombea kiti cha ubunge Imenti Kaskazini) na John Mutunga (Tigania Magharibi).

You can share this post!

Bahati itaendea nani?

Mafuriko: Watu 63 bado hawajajulikana waliko

T L