Habari za Kitaifa

Nyota wa Malkia Strikers Janet Wanja afariki, familia yatangaza

Na BENSON MATHEKA December 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA nyota wa timu ya Taifa ya voliboli Malkia Strikers, Janet Wanja, ameaga dunia wiki chache tu baada ya familia yake kufichua kuwa alikuwa akiugua saratani ya kibofu cha nyongo.

Kifo cha Wanja kilithibitishwa jioni ya Alhamisi, Desemba 26, na familia yake, ambayo ilitoa taarifa ikisema kuwa alifariki kutokana na ugonjwa huo.

“Familia ya Janet Wanja ingependa kutangaza kifo chake baada ya kuugua saratani,” taarifa kutoka kwa mmoja wa wanafamilia yake ilisema.

Katika taarifa hiyo hiyo, familia pia iliishukuru kampuni ya Kenya Pipeline, ambayo ilijitolea kugharamia bili zake za matibabu kwa asilimia 100 mapema mwezi Desemba baada ya kuomba msaada wa kifedha ili kumsaidia katika matibabu.

Wanja alikuwa mmoja wa wachezaji waliokaa muda mrefu zaidi kwenye timu ya voliboli ya Kenya Pipeline, akicheza kuanzia 2005 hadi alipostaafu 2019.

Taarifa ya familia iliendelea, “Shukrani zetu za dhati ziende kwa kampuni ya Kenya Pipeline kwa kutembea nasi tangu mwanzo na kutoa msaada wa matibabu bila kuchoka.”

Kifo cha Wanja kimetokea kama mshtuko kwa wadau wa michezo huo nchini Kenya, ambao walikuwa na matumaini kwamba angekabiliana na ugonjwa wa saratani.

Miongoni mwa waliomwomboleza ni mchezaji wa Harambee Stars na Al-Duhail Michael Olunga. “Umeondoka haraka sana. Mchango wako kwa Voliboli nchini Kenya na sekta ya michezo ulikuwa mkubwa,” akasema.

Rais William Ruto pia alimuomboleza nguli huyo wa Malkia Strikers, akimtaja kama shujaa wa kitaifa.

“Janet Wanja, nyota wa voliboli mwenye kipawa na nidhamu, alitumikia nchi yetu kwa heshima na kujitolea. Nafariji familia yake, marafiki katika wakati huu mgumu,” alisema.

Wanja alikuwa katika timu iliyowakilisha Kenya kwenye michezo ya Olimpiki, Athens mwaka wa 2004.

Mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Upili ya Mukumu Girls, Wanja pia aliiongoza timu ya taifa ya voliboli chini ya usimamizi wa Sammy Kirongo.

Baada ya kustaafu, alibadilika na kuwa kocha, na kuchukua jukumu kama mkufunzi wa washambuliaji wa Malkia.