ODM inavyomezea mate minofu katika serikali ya Ruto
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga, kinajiandaa kwa mazungumzo ya kitaifa yaliyoitishwa na Rais William Ruto kikilenga kushinikiza mabadiliko makubwa serikalini.
Chama hicho kinaamini kuwa, mapendekezo ya Jukwaa la Kitaifa la Sekta Mbalimbali na mazingira ya sasa ya kisiasa ambayo yamemzonga Rais Ruto, yanatoa fursa kwa serikali kutekeleza mabadiliko, ambayo baadhi yamekwama Bungeni.
Kulingana na mpango huo, wanasema ikiwa Rais Ruto ataachwa ajiondoe katika mzozo wa sasa wa kisiasa unaokabili utawala wake peke yake, baadhi ya mageuzi yanayoletwa na upinzani, ikiwa ni pamoja na mageuzi ya uchaguzi huenda yasitekelezwe.
“Hatupaswi kuruhusu hili lipite peke yake, lazima tuchukue fursa hiyo kusukuma mageuzi ya maana ambayo chama kinasimamia,” alisema afisa mkuu wa chama cha ODM.
Chama hicho kilikaribisha kutiwa saini kwa Mswada wa Marekebisho wa IEBC, 2024 na Rais Ruto Jumatano lakini sasa kinapanga njama ya kuharakishwa kwa Miswada minane iliyosalia ya Nadco.
“Huu ndio wakati mwafaka wa kushinikiza mageuzi, kutiwa saini kwa Mswada wa IEBC ni hatua nzuri,” afisa huyo alisema.
Katika taarifa baada ya mkutano wa Kamati Kuu Simamizi ya chama hicho jana, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema japo wako tayari kwa mazungumzo ya kitaifa yaliyoitishwa na Rais Ruto, angemtimua kwanza Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome na kamanda wa Polisi Nairobi Adamson Bunge.
Na jana, Rais Ruto alitangaza kujiuzulu kwa Bw Koome.
Chama hicho pia kilitaka maafisa wote wa polisi waliohusishwa na mauaji ya Wakenya zaidi ya 200 wasio na hatia katika maandamano ya amani tangu mwaka jana wakamatwe.
Aidha, chama hicho pia kinadai msamaha wa kitaifa kwa watu wote waliokamatwa au kushtakiwa kuhusiana na maandamano, na fidia kwa waathiriwa wote wa ukatili wa polisi.
“Uamuzi wa kutimua baraza lake la mawaziri ulikuwa mwanzo mzuri kwa maoni yetu. Lakini hisia kote nchini ni kwamba bado kuna hali ya woga ambayo inafanya watu kutozungumza kwa uhuru. Ruto lazima amtimue IG wa Polisi mara moja, kamanda wa Polisi wa Nairobi na kuwakamata maafisa wote wa polisi wanaohusishwa na mauaji ya Wakenya zaidi ya 200 wasio na hatia katika maandamano ya amani tangu mwaka jana,” Bw Sifuna alisema.
Wakati wa kutiwa saini kwa Mswada huo ambao ulikuwa wa kwanza kati ya tisa iliyotoka kwa kamati ya NADCO, kiongozi wa Upinzani Raila Odinga alisema ikiwa ripoti hiyo inaweza kutekelezwa kikamilifu, basi serikali inaweza kutatua msukosuko wa sasa.
“Ripoti ya NADCO ina masuala mengi sana ambayo ni maoni ya Wakenya wengi leo, ukiona masuala yanayoibuliwa na vijana, mengi yao yako kwenye ripoti ya Nadco,” Bw Odinga alisema.
Chama hicho jana kilifafanua kuwa uamuzi wao wa kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa haufai kuchukuliwa vibaya kumaanisha wanajiunga na serikali inayozama ya utawala wa Kenya Kwanza.
“Masuala yanayoibuka na hitaji la dharura la kuyashughulikia si kuhusu kunusuru utawala wa Kenya Kwanza. Taifa ni kubwa kuliko kila mmoja kati yetu. Tunaona hii kama nafasi ya kuliokoa Taifa letu lisiporomoke,” Bw Sifuna alisema.
“Tunaamini katika kupiga vita dhuluma na udikteta kwa sababu tunaamini kila raia wa nchi ana haki ya kutoa maoni hayo na kusikilizwa. Mgogoro huu wote ulichochewa na kushindwa kusikiliza,” aliongeza seneta huyo wa Nairobi.
Hata hivyo, bado haijabainika iwapo chama hicho kinajiandaa kuteua baadhi ya wanachama wake kujiunga na Baraza la Mawaziri katika ‘serikali pana’ ambayo Rais Ruto alisema atajiunga nayo Alhamisi.
Alipoulizwa na ‘Taifa Leo’ ikiwa chama hicho kitakubali nafasi za baraza la mawaziri iwapo zitatolewa katika Baraza jipya la Mawaziri, Bw Sifuna alisema wataenda kwenye meza ya mazungumzo ya kitaifa kwanza.