Onyo kuhusu mvua kubwa Nairobi, Mombasa na maeneo mengine kadhaa kwa siku mbili
WAKENYA wanaoishi kaunti za Nairobi, Mombasa, Embu na Tharaka Nithi, wameonywa kuwa mvua kubwa inatarajiwa kunyesha maeneo hayo Alhamisi, Novemba 14 na Ijumaa, Novemba 15.
Idara ya Utabiri ya Hali ya Hewa ya Kenya imeonya Wakenya kwamba mafuriko yanaweza kutokea katika siku hizi mbili katika maeneo hayo.
“Mvua ya zaidi ya milimita 20 inatarajiwa kunyesha katika muda wa saa 24 kuanzia Alhamisi, Novemba 14, katika sehemu za Bonde la Ufa, Kati ikijumuisha Nairobi na nyanda za Kusini Mashariki.
“Mvua hiyo huenda ikaongezeka hadi milimita 30 Ijumaa, Novemba 15, katika nyanda za kusini mashariki na sehemu za kati ikiwa ni pamoja na eneo la Nairobi,”ilisema sehemu ya taarifa ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya.
Kaunti zingine ambazo zinaweza kukumbwa na mvua kubwa ni pamoja na; Meru, Kirinyaga, Murang’a Nyeri Kiambu, Nyandarua, Laikipia, Isiolo, Kericho, Bomet, Narok sehemu za Kajiado, na Makueni.
Wakenya wanaoishi chini ya mito na kando ya mito ya msimu wameshauriwa kuwa waangalifu kwani maji yanaweza kutokea ghafla ingawa mvua inaweza kukosa kunyesha katika maeneo hayo.
Watu pia wameonywa dhidi ya kuendesha gari na kutembea kwenye mvua kwa usalama wao.
Wale wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na hatari ya maporomoko ya ardhi, haswa Aberdare, Mlima Kenya, na maeneo mengine yenye milima wameshauriwa kuwa waangalifu.
Mapema wiki hii, idara hiyo ilionya kuhusu usiku wa baridi katika maeneo kadhaa. Ushauri huo ulibainisha kuwa joto la usiku lilitarajiwa kushuka hadi nyusi 10°C wiki hii, kabla ya kupanda hadi nyusi 11°C kuelekea wikendi.
Katika tangazo lake, idara iliwataka wakazi wa Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet kujiandaa na halijoto ya juu ya mchana ya hadi 33°C.
Kaunti zingine ambazo zilitahadharishwa kujiandaa kwa siku za joto ni pamoja na Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia, Pokot Magharibi, Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, Isiolo, Mombasa, Tana River, Kilifi, Lamu na Kwale.