Habari za Kitaifa

Passaris aahidi kutetea kortini familia ya mgonjwa aliyeuawa wodi KNH  

Na SAMMY WAWERU February 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE mwakilishi wa Kaunti ya Nairobi, Esther Passaris ameahidi kuwakilisha kortini familia ya mgonjwa aliyeuawa kwenye wodi Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Gilbert Kinyua, 39, alipatikana kwenye wodi ya KNH akiwa amefariki usiku wa kuamkia Ijumaa, Februari 7, 2025.

Alikuwa amelazwa wodi 7B.

Kulingana na wahudumu wa afya waliokuwa kwenye zamu, Kinyua alikuwa amefunikwa kwa shuka iliyoloa damu akiwa na majeraha ya kukatwa shingoni.

Huku idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) ikiendeleza uchunguzi, Bi Passaris ambaye ni mbunge mwakilishi wa kike Nairobi ameahidi endapo KNH haitalipa familia ya marehemu fidia, atawawakilisha kortini.

“Ninahitaji kujua ikiwa KNH itafidia familia ya marehemu… Endapo itafikia mahali suala hili lielekee kortini kutafuta haki, na jinsi taratibu za korti huwa ndefu, nitawaandikia wakili wa kuwapigania haki,” Bi Passaris alisema.

Mbunge huyo wa ODM, alitoa hakikisho hilo mnamo Jumanne, Februari 11, 2025 baada ya kutembelea familia ya mwathiriwa Nairobi.

Kinyua, alikuwa mume na baba.

“KNH inapaswa kuelewa kwamba hii ni familia changa na ina watoto wawili wadogo,” Bi Passaris alielezea.

“Hata hivyo, ninatumai kuwa tutasuluhisha suala hili nje ya korti, ili familia ya marehemu isihangaike kupata haki. Baadhi ya kesi huchukua hata muda wa miaka kumi maamuzi kufanywa.”

Passaris alihimiza DCI kufanya uchunguzi wa kina, na kwa haraka ili walioangamiza Kinyua wapatikane na kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

Kwenye kikao na wanahabari mnamo Jumapili, Februari 9, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji KNH, William Sigilali alithibitisha mauaji hayo kutekelezwa kwenye wodi ya hospitali hiyo ya kitaifa, Nairobi.

“Hatuna ushahidi kuonyesha kwamba kuna yeyote aliyetoka nje na kuangamiza mgonjwa. Aliuawa akiwa kwenye wodi,” afisa huyo alisema, akidokeza kwamba kesi hiyo imetwaliwa na makachero wa DCI.

Kisa hicho cha mgonjwa kuuawa kwenye wodi, kimeibua usalama wa wagonjwa hospitalini hasa waliolazwa.