Mhubiri azua gumzo kukataa sadaka ya Sh100,000 ya mbunge
MCHUNGAJI maarufu wa Nairobi, Peter Manyuru, amezua gumzo baada ya kukataa mchango wa Sh100,000 kutoka kwa Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la Jesus Teaching Ministry, Embakasi.
Katika tukio hilo la kushangaza, Mbunge Amisi alikuwa amesimama tayari kuwasilisha mchango wake, lakini Mchungaji Manyuru alimkatiza na kusema kuwa kanisa lake halitapokea tena pesa kutoka kwa wanasiasa, hatua iliyopokelewa kwa makofi na nderemo kutoka kwa waumini waliokuwepo.
“Najua baadhi yenu mko hapa kwa mara ya kwanza tangu tuliposema hatutapokea pesa kutoka kwa wabunge. Hatutaki kusemwa kuwa tunahongwa. Badala yake, tuko tayari kujiunga nanyi kwenye harambee zenu huko nje ya kanisa,” alisema mchungaji Manyuru kwa msisitizo.
Uamuzi huu wa kanisa umeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kulinda heshima na uadilifu wa madhabahu, kufuatia malalamishi ya umma kuwa makanisa yanatumika kama njia ya kuhalalisha pesa zisizoeleweka chanzo chake.
Tukio hili lilitokea mbele ya viongozi kadhaa wa muungano mpya wa kisiasa unaojulikana kama Kenya Moja Alliance, wakiwemo Seneta Edwin Sifuna (Nairobi) na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, ambao walihudhuria ibada hiyo.
Wakati wa ibada hiyo, viongozi wa Kenya Moja walitumia jukwaa hilo kupigia debe umoja wa upinzani na kutangaza nia ya kuungana na viongozi kama Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, George Natembeya na Fred Matiang’i ili kumshinda Rais Ruto mwaka 2027.
Hata hivyo, hatua ya Mchungaji Manyuru ya kufunga milango kwa michango ya kisiasa imeibua mazungumzo mapya kuhusu uhusiano kati ya siasa na dini, huku wananchi wengine wakitaka makanisa mengine yafuate mfano huo ili kulinda uaminifu wao mbele ya waumini na jamii kwa jumla.