Habari za Kitaifa

Pigo kwa Raila Somalia ikimruka kuhusu kumuunga kwa kiti cha AUC

Na JUSTUS OCHIENG November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga ameanza kampeni zake za kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) katika eneo muhimu la Afrika Magharibi, huku kukiwa na ripoti kwamba Somalia imemruka.

Hatua ya Somalia ni doa katika azma yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo awali iliidhinisha kugombea kwake kama kanda.

Bw Odinga aliwasili Cotonou, Benin, ambako alifanya mazungumzo Alhamisi na waziri wa masuala ya kigeni wa taifa hilo la Afrika Magharibi, Olushegun Adjadi Bakari.

Haya yanajiri huku ikibainika kuwa Somalia, mojawapo ya nchi nane wanachama wa EAC zilizomuidhinisha wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni zake katika Ikulu ya Nairobi mnamo Agosti 27, itampigia kura mpinzani wake mkuu, Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Mahmoud Youssouf, katika uchaguzi wa Februari 2025.

Bw Odinga anashindana na Bw Youssouf, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Nje wa Mauritius Anil Kumarsingh Gayan na mwenzake wa zamani wa Madagascar Richard James Randriamandrato katika uchaguzi huo.

EAC ina nchi nane wanachama zikiwemo; Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Sudan Kusini na Somalia.

Mwenyekiti wa EAC Salva Kiir Mayardit ambaye pia ni rais wa Sudan Kusini aliongoza marais wa kanda kumuidhinisha Bw Odinga kwa wadhifa huo wa juu zaidi barani Nairobi mnamo Agosti.

Rais Mayardit, na wenzake wa EAC Yoweri Kaguta Museveni (Uganda), Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Waziri Mkuu wa Burundi Gervais Ndirakobuca, mwakilishi wa Rais wa Rwanda Paul Kagame – Waziri wa Masuala ya Nje James Kabarebe wote walitangaza kwamba nchi zao zinamuunga mkono Bw Odinga.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Ruto ambaye pia aliwasilisha radhi ya Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisisitiza kujitolea kwa pamoja kwa mshikamano na utangamano katika Afrika Mashariki.

“Eneo letu la Afŕika Mashaŕiki, ambalo ni makazi ya zaidi ya watu 500 milioni linachukulia wakati huu kuwa zamu yake ya kutoa uongozi kwa bara,” Rais Ruto alisema wakati huo.

Ingawa Dkt Ruto alikuwa amewasilisha pole za rais wa Somalia wakati wa uzinduzi wa kampeni za Bw Odinga, serikali  ya nchi hiyo sasa imethibitisha kuwa “ilikuwa na ahadi ya awali na Djibouti,” kuhusu nafasi ya AUC.

Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni Dk Korir Sing’oei aliambia Taifa Leo kwamba wakati wa Kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York mnamo Septemba, alikutana na Makatibu  kutoka nchi za EAC ambao waliamua kuunga mkono kampeni za Kenya.

“Nchi zote zilizokuwepo ziliunga mkono hilo isipokuwa Somalia ambayo iliunga mkono maafikiano hayo lakini ikaashiria kwamba ilikuwa imeahidi hapo awali kuunga Djibouti kabla ya Mheshimiwa Odinga kutangaza kuwania kiti hicho,” alisema Dkt Sing’oei.

Alibainisha Bw Odinga alitangaza azma yake baada ya mgombeaji kutoka Djibouti alikuwa tayari ametangaza azma yake.

“Kwa hivyo, Somalia iliwasilisha kwa kamati kwamba imefungwa na ahadi hiyo lakini hata hivyo, iliunga mkono kikamilifu maafikiano ya kanda kuunga mkono Bw Odinga. Hayo kwetu ni maendeleo muhimu sana na tunapeleka ripoti kwa kamati ya baraza la mawaziri kwa ushauri zaidi,” aliongeza.

Hatua hiyo ya Somalia ni pigo kwa Bw Odinga, ambaye alikuwa ameungwa mkono na aliyekuwa waziri wa masuala ya kigeni wa nchi hiyo, Fawzia Yusuf, ambaye alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho mapema Agosti.

“Nina furaha kutangaza kumuunga mkono Mheshimiwa Raila Odinga katika azma yake ya kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika” Bi Fawzia alisema baada ya kukutana na Bw Odinga mnamo Agosti 9.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA