Habari za Kitaifa

Pigo kwa wabunge korti ikiamua CDF ni haramu

Na CHARLES WASONGA September 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu imeamua kuwa Sheria ya Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) ya 2015 inakiuka Katiba.

Kwenye uamuzi walioutoa Ijumaa, Septemba 20, 2024 Majaji Kanyi Kimondo, Mugure Thande na  Roselyne Aburili, hata hivyo, walitoa muda wa hadi Juni 30, 2026 kabla sheria hiyo kukoma kutumika kabisa.

Walisema wametoa nafasi hiyo ili kutoa nafasi ya kukamilishwa kwa miradi na mipango iliyoanzishwa katika maeneo bunge 290 kwa ufadhili wa pesa za hazina hiyo.

“Tunafahamu kwamba kuna miradi yenye kutekelezwa kwa vipindi mbalimbali chini ya hazina hii. Sasa mwaka wa kifedha umeanza na ni wazi kuwa pesa zilikuwa zimetengwa kwa miradi hiyo,” majaji hao watatu wakasema katika uamuzi wao.

Kesi hiyo iliwasilishwa na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Wanjiru Gikonyo na Cornelius Oduor.

Wawili hao walisema kuwa Sheria ya NG-CDF inaunda ngazi ya tatu ya utawala, hali ambayo ni kinyume cha sheria.

Aidha, walisema kuwa sheria ya NG-CDF inakiuka kanuni ya utengano wa kimamlaka kati ya nguzo za serikali.

Kulingana na Bi Gikonyo na Oduor kuhusishwa kwa wabunge katika hazina ya NGCDF kunaathiri kanuni ya utengano wa kimlaka kwani kunaathiri mamlaka ya serikali kuu na mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Umma (PSC).

Aidha, walisema kuwa sheria hiyo, ya NG-CDF inaingilia kanuni ya utengano wa kimajukumu kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti.

Isitoshe, Bi Gikonyo na Bw Oduor walisema kuwa Sheria ya NG-CDF ilitungwa bila kuhusishwa na Bunge la Seneti “ilhali inatumika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya serikali za kaunti.”

Hata hivyo, akitetea sheria hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Hazina ya NG-CDF Musa Sirma alisema kuwa hazina hiyo inatekeleza manufaa makubwa zaidi kwa wananchi, haswa katika ngazi za mashinani.

“Ikiwa NG-CDF itafutiliwa mbali haki za kiuchumi na kijamii za wananchi zitakuwa zimekiukwa,” akasema Mbunge huyo wa Eldama Ravine.