Habari za Kitaifa

Polisi wa Kenya alivyotoweka Haiti

Na NYABOGA KIAGE March 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

OPERESHENI ya kuondoa gari la polisi lililokwama kwenye mtaro iliishia afisa mmoja wa kikosi cha Kenya kinachohudumu Haiti kupotea.

Gari hilo, linalomilikiwa na Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP), lilikuwa kwenye doria ya kawaida Jumanne, Machi 25 lilipokwama kwenye mtaro unaoshukiwa kuchimbwa na magenge kwenye barabara kuu ya Carrefour Paye-Savien huko Pont-Sonde.

HNP iliwaarifu maafisa wanaohudumu chini ya Kikosi cha Usalama wa Mataifa Mbalimbali (MSS) kinachoongozwa na Kenya, ambao walijibu haraka.

“Ili kusaidia katika uokoaji, magari mawili ya MSS kutoka Pont-Sonde yalitumwa. Kwa bahati mbaya, moja pia lilikwama huku jingine likipata hitilafu ya kiufundi,” msemaji wa MSS, Bw James Ombaka, alisema katika taarifa.

Tatizo hilo liliwalazimu maafisa waliokuwa kwenye gari la HNP kushuka na kujaribu kutatua hali hiyo.

Walipokuwa wakishughulika, washukiwa wa genge waliokuwa wakiwavizia waliwashambulia ghafla.

Kulingana na Bw Ombaka, mmoja wa maafisa wa MSS wa Kenya alipotea baada ya shambulio hilo.

“Timu maalum zimetumwa kufanya msako na kubaini alipo,” Bw Ombaka alisema.

Kenya inaongoza mataifa mengine katika nchi hiyo ya Caribea katika operesheni ya kurejesha utulivu na kukomesha magenge ambayo yamekuwa yakisababisha ghasia kwa miaka mingi.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari/taarifa-za-kuuawa-kwa-polisi-haiti-zafikishwa-kijijini-kwao-kajiado-na-kuacha-simanzi-kuu/

Kupotea kwa afisa huyo wa Kenya kulivutia hisia kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini Nairobi, ambayo ilisema kuwa inafuatilia kwa karibu suala hilo.

“MSS kwa kushirikiana na HNP inaendesha operesheni kumtafuta ili kumpata afisa aliyepotea,” msemaji wa polisi wa Kenya, Bw Michael Muchiri, alisema.

Kikosi cha kwanza cha maafisa wa Kenya kilifika Haiti mnamo Juni 2024.

Tangu wakati huo, afisa mmoja tayari amepoteza maisha akiwa kazini.

Samuel Tompoi Kaetuai aliuawa kwa kupigwa risasi mnamo Februari 23 na mshukiwa wa genge ambaye pia alipigwa risasi na maafisa wa polisi.

Marehemu alizikwa nyumbani kwake Kajiado mnamo Machi 19.

Kenya ilituma maafisa zaidi wa polisi nchini Haiti licha ya kupunguzwa kwa bajeti iliyotangazwa na Rais wa Amerika Donald Trump.

Serikali ya Amerika ilisitisha ufadhili wa Sh1.7 bilioni uliokuwa umepangwa kwa operesheni hiyo, lakini siku chache baada ya tangazo hilo, Kenya ilipeleka maafisa wengine 144 Haiti.

Awali, Amerika ilikuwa imejitolea kutoa Sh1.9 bilioni kufikia wakati wa tangazo la kusitisha ufadhili, ni Sh219 milioni pekee zilizokuwa zimetumika.

Maafisa wa Kenya walioko Haiti wanatoka katika vitengo vya Huduma ya Polisi ya Kenya kama vile Kikosi cha Kukabiliana na Fujo (GSU), Kitengo cha Kupambana na Wizi wa Mifugo, Kitengo cha Kukabiliana na Dharura, na pia kikosi maalum cha Wanawake cha Silaha na Mbinu za Kivita (SWAT Team).

Mbali na Kenya, nchi zingine zilizopeleka maafisa wao Haiti ni Jamaica, Belize, Bahamas, Guatemala, na El Salvador.