Presha kwa Raila ‘ground’ ikitaka amtaliki Ruto
KINARA wa ODM Raila Odinga anakabiliwa na presha kutoka ngome yake ya Nyanza avunje ndoa yake ya kisiasa na Rais William Ruto kuokoa sifa yake kama mwanamageuzi.
Kauli za Gavana wa Siaya James Orengo na mwenzake wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyongó kuhusu utawala wa Rais William Ruto wa Kenya Kwanza umeamsha shinikizo za kumtaka Bw Odinga ajiondoe serikalini.
Aidha uteuzi wa Jaoko Oburu, mpwa wa Bw Odinga na mwanawe Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga, kama mshauri wa kiuchumi wa Rais Ruto umetonesha kidonda.
Uteuzi huo umeamsha ghadhabu mitandaoni hasa baadhi ya vijana wanaotoka Nyanza wakidai Serikali Jumuishi ni ya kutimiza maslahi ya kibinafsi ya familia ya Bw Odinga.
Baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo ilizinduliwa na nyingine kuahidiwa na Rais pia imekuwa kiazi moto huku raia wakionekana kutoamini kama itatekelezwa na kukamilika kwa wakati.
Mgawanyiko ambao umeibuka ndani ya ODM kuhusu kufanya kazi na serikali nao kunazua maswali iwapo Raila atauhimili na kusimama na Rais hadi 2027.
Mnamo Jumanne, Gavana Nyongó aliwakia Rais Ruto akisema utawala wake unalenga kurejesha taifa nyuma na kuondoa faida ambayo imepatikana tangu ukombozi wa pili upatikane kuelekea kura ya 1992.
Gavana huyo alionekana kukerwa na hatua ya serikali kukataa kuwaachia magavana kusimamia pesa za ujenzi wa barabara huku akisema hilo halifai ikizingatiwa kwamba kaunti zimekuwa zikisimamia vyema sekta ya afya.
“Ukweli ni kwamba utawala wa Ruto umeamua kulirejesha taifa nyuma kwenye enzi ambazo hakukuwa na ugatuzi. Matunda ambayo yamepatikana kupitia ukombozi wa pili hayafai kuachwa yapotee tu vivi hivi,” akasema Profesa Nyongó.
Kauli ya Profesa Nyongó dhidi ya serikali imeamsha madai yaliyokwepo kuwa Gavana huyo alikuwa akipinga hatua ya ODM kubuni ushirikiano na Rais Ruto na hata alikataa nafasi ya uwaziri.
Profesa Nyongó amekuwa mwandani wa Raila kwa miaka mingi na hata wakati ambapo kinara huyo wa upinzani alikuwa akiwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), ndiye aliachiwa uongozi wa ODM.
Gavana huyo anayehudumu muhula wake wa pili pia alihudumu kama Katibu Mkuu wa ODM wakati ambapo chama hicho kilibuniwa mnamo 2005 hadi 2014 na ni kati ya wanasiasa ambao hawajawahi kuterereka kwenye uaminifu wao kwa Bw Odinga.
Gavana Orengo wakati wa mazishi ya mlinzi wa Raila mnamo Aprili 12, alizua mdahalo ambapo alisema hawezi kuwa kibaraka wa Rais Ruto
“Mimi siwezi kuwa kibaraka kwa sababu tulipigania katiba ambayo watu wanaruhusiwa kuzungumza. Nilikuwa bunge ambalo wabunge walikuwa wakimwaambia Rais Daniel Moi kuwa hakuna mahali ataenda na angeongoza milele,” akasema Bw Orengo.
“Mkiendelea kuwa kibaraka hatutakuwa na nchi. Waambieni viongozi wenu ukweli na mimi siimbii mtu kwa sababu lugha ambayo nimesikia hapa, inaashiria kuwa nchi hii inapoteza hadhi yake,” akaongeza.
Uteuzi wa Bw Jaoko kama mshauri ulizua kejeli mitandaoni, baadhi wakidai kuwa anatosha kwa wadhifa huo mradi amehitimu huku wengine wakisema ametunukiwa wadhifa huo kutokana na ushirikiano kati ya Bw Odinga na Rais.
Ishara kuwa hata bungeni ushirikiano wa Raila na Ruto si shwari ulidhihirika wakati ambapo Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed mnamo Aprili 18 alipinga baadhi ya wanasiasa kuteuliwa kama mabalozi baada ya kufutwa serikalini.
“Watumishi wa umma watapata nafasi lini kupiga hatua kitaaluma iwapo tutakuwa tukiwachukua wanasiasa walioshindwa au kufutwa na kuwateua kama mabalozi. Kiongozi wa wengi (Kimani Ichung’wah) hakuna cha serikali jumuishi hapa, niruhusu nifanye kazi yangu,” akasema Bw Mohamed.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati inaonekana meli ya Raila na Rais imeanza kuyumbayumba kwa sababu wananchi wanauliza wananufaika aje ilhali changamoto na sera hasi zimesalia zile zile.
“Kulipuka kwa Orengo na Nyongó ambao wamekuwa na Raila miaka hii yote si jambo la kupuuzwa, lazima wametambua kitu na yaliyomo kwenye mkataba huenda hayatatekelezwa.
“Pia Rais amekuwa akifungua miradi Nyanza lakini inaonekana utekelezaji wake hauendelei jinsi wengi walivyotarajiwa nao vijana wanauliza wananufaika kivipi iwapo jamaa za viongozi ndio wanapewa kazi wao wakikabiliwa na matatizo yale yale,” akasema Andati.
Mchanganuzi huyo anasema kuwa inaonekana wabunge wa ODM watapata ugumu wa kuuza serikali jumuishi Nyanza na maeneo mengine kwa sababu upinzani wa Bw Orengo umefanya raia wazinduke kuhusu uongozi wa Rais Ruto.