Habari za Kitaifa

Raila, anayesaka kiti cha AUC kwa udi na uvumba, kuzindua kampeni rasmi Ethiopia

Na JUSTUS OCHIENG’ October 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KENYA imepanga mikutano kadhaa ya kumpigia debe Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ambaye anawania kiti cha Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) katika uchaguzi wake utakaoandaliwa Februari 5 mwaka ujao.

Bw Odinga anatarajiwa kuzindua azma yake jijini Addis Ababa Ethiopia mnamo Novemba 8, miezi miwili baada ya kuandaa ile ya ukanda wa Afrika Mashariki mnamo Agosti 27.

Rais William Ruto aliwaongoza Marais Salva Kiir Mayarditi (Sudan Kusini) ambaye pia ni mwenyekiti wa EAC kumuidhinisha Bw Odinga kuwa mwaniaji bora wa uenyekiti wa AUC.

Wengine ambao walihudhuria sherehe hiyo iliyoandaliwa ikulu ya Nairobi ni Marais Yoweri Museveni (Uganda), Samia Suluhu (Tanzania), Waziri Mkuu wa Burundi Gervais Ndirakobuca, mwakilishi wa Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye ni Waziri wa Masuala ya Nje James Kabarebe.

Kikosi cha Bw Odinga kimefunguka na kusema kuwa mipango inaendelea kukamilishwa kuelekea uzinduzi huo ambao utafanyika katika makao makuu ya AU mwezi ujao.

“Mwaniaji wetu Raila alikuwa Addis mnamo Jumatatu na tumetenga Novemba 8 kama siku ambayo atazindua kampeni yake ya uenyekiti wa AUC, Addis Ababa. Ndiye kiongozi wa kuhakikisha kuwa AU inatimiza ajenda na malengo yake kufikia mnamo 2063,” akasema Elkanah Odembo ambaye ni mwenyekiti wa sekretariati ya kampeni za Bw Odinga.

Alisema uzinduzi wa kampeni za Bw Odinga utaonyesha nia yake ya kuhakikisha kuwa AU inafikia hadhi ya miungano ya mabara mengine.

Bw Odembo ambaye ni balozi wa zamani wa Kenya nchini Amerika, pamoja na Katibu katika wizara ya masuala ya kigeni Dr Sing’oei wanaongoza kikosi cha kampeni za Bw Odinga.

Wawili hao wanashikilia kuwa waziri huyo mkuu wa zamani amezidisha juhudi za kutwaa uenyekiti wa AUC.

“Raila anapanga kuhutubia kongamano la mataifa wanachama wa Comesa litakalofanyika Oktoba 31 kule Bujumbura, Burundi,” akasema Bw Odembo COMESA, muungano wa kiuchumi wa mataifa ya mashariki na kusini mwa Afrika ina wanachama 21, idadi ambayo Bw Odembo anasema Raila akijihakikishia, basi ana uhakika wa kushinda uenyekiti wa AUC.

Mnamo Novemba 5, siku tatu kabla ya uzinduzi huo, Bw Odinga atahudhuria Kongamano la Kawi jijini Cape Town Afrika Kusini kabla ya kuelekea COP29, Baku, Azerbaijan kati ya Novemba 16 – Novemba 20.

Bw Odembo pia alifichua kwamba sekretariati imempangia Raila ratiba kali ambapo anatarajia kutembelea mataifa sita na kujipigia debe ndani ya wiki nne zijazo.

“Miji mikuu ambayo atafika katika muda huo ni Abidjan (Côte d’Ivoire), Porto-Novo (Benin), Dakar (Senegal), Abuja (Nigeria), Algiers (Algeria) na Gaborone (Botswana),” akasema Bw Odembo.