Habari za Kitaifa

Raila atetea dili za Adani akisema ameijua kampuni hiyo tangu akiwa Waziri Mkuu

Na VALENTINE OBARA October 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ametetea kupewa kwa kandarasi za JKIA na kawi kwa kampuni ya Adani, akisema ina uwezo wa kuleta ufanisi akitoa mifano ya dili kama hizo Mumbai na Gujarat.

Waziri Mkuu huyo wa zamani hata hivyo ameitaka serikali kuunda kanuni mahsusi za kusimamia mikataba baina ya serikali na kampuni za kibinafsi.

Bw Odinga alitoa mapendekezo kadhaa kwa serikali ya Kenya Kwanza, huku akisisitiza kwamba ODM si sehemu ya serikali inayotawala.

Chama hicho kimekuwa kikihusishwa na serikali haswa baada ya viongozi wake watano kujumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri.

Raila ambaye ameepuka kuzungumzia masuala ya kitaifa tangu aanze kampeni za kugombea Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), Jumapili alijongea gumzo kuhusu dili za Adani, kuundwa kwa Tume ya Uchaguzi na kutekwa nyara kwa watu wanaofikiriwa kuwa wakosoaji wa serikali.

Bw Odinga alitaka sheria iheshimiwe. Katika kipindi fulani wakati wa mkutano huo na wanahabari, Raila alibubujikwa na machozi akielezea jinsi katiba ilipiganiwa kwa hali na mali akisisitiza kwamba ilindwe kwa njia yoyote ile.

Kulingana na Bw Odinga, kampuni ya Adani inaheshimika kimataifa lakini ujio wake nchini unaweza kuwa unaathiriwa na ukosefu wa mipangilio sahihi ya kisheria.

Alisema kwamba kampuni hiyo imekuwa ikionyesha nia ya kutaka kuwekeza nchini tangu 2010 akiwa Waziri Mkuu wakati wa serikali ya Mwai Kibaki.

Ingawa amesifu uwezo wa kampuni hiyo, anasema ukosefu wa sera za kisheria kwa sasa utafanya iwe vigumu kulinda maslahi ya umma na ya wawekezaji wa kimataifa.

Kampuni hiyo ya India imezua mjadala kuhusiana na mpango wa kukodisha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa miaka 30.

Kampuni hiyo pia imehusishwa na Sh104  bilioni za mpango mpya wa afya kwa wote (UHC) kupitia kwa Apiero Limited.