Raila kuaga siasa za Kenya kesho, Jumanne
KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga kesho, Jumanne, Agosti 27, 2024 anatarajiwa kuaga rasmi siasa za Kenya ambapo uwanizi wake wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) utazinduliwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Rais Ruto, baraza lake lote la mawaziri, maafisa wa ngazi za juu serikalini, kesho asubuhi watakongamana katika Ikulu ambapo azma ya Bw Odinga itazinduliwa na kuhudhuriwa na Marais kutoka nje ya nchi pia.
Uchaguzi wa AUC utaandaliwa Februari 2025 na kiongozi huyo wa ODM anaonekana kama mwanasiasa ambaye yupo kifua mbele kuwahi kiti hicho.
Juhudi za kumrithi mwenyekiti wa sasa Moussa Faki Mahamat zinaonekana kushika kasi huku kampeni za Raila zikipigwa jeki baada ya Fawzia Yusuf, waziri wa zamani wa nje wa Somalia akijiondoa kwenye kinyang’anyiro cha AUC.
Waziri Mkuu huyo wa zamani mwenyewe atakuwa akiaga siasa za Kenya katika Ikulu jumba ambalo amejaribu kuishi bila mafanikio baada ya kubwagwa kwenye kinyang’anyiro cha urais mnamo 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022.
Leo, Jumatatu, Agosti 26, 2024, ilibainika kuwa zaidi ya marais watano watakuwa katika Ikuluni katika hafla ya kuzindua azma ya Raila ambaye sasa ataanza safari kuzunguka mataifa 54 ya Bara Afrika akisaka uungwaji mkono.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Salva Kiir Mayardit (Sudan Kusini), Samia Suluhu (Tanzania), Hassan Sheikh Mohamud (Somalia), Waziri Mkuu wa Burundi Gervais Ndirakobuca na Waziri wa Masuala ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe kufikia leo walikuwa wamethibitisha kuwa watakuwa katika hafla hiyo.
Wizara ya Masuala ya Nje pia ilithibitisha kuwa Marais wote wa ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamealikwa katika Ikulu ya Nairobi kuhudhuria hafla ya kuvumishwa kwa Raila Barani Afrika.
Aliyekuwa Rais wa Nigeria Olesegun Obasanjo ambaye aliandamana na Raila kwenye tamasha za tano za FESTAC zilizofanyika Kisumu Jumatau, Agosti 26, 2024, pia anatarajiwa kuwa Ikulu kushuhudia Raila akianza safari ya kuwania kiti hicho cha AUC.
Ni Bw Obasanjo, rafiki mkubwa wa babake Raila, marehemu Jaramogi Oginga Odinga, aliandamana na kiongozi huyo wa ODM alipotangaza kuwa ananyemelea uenyekiti wa AUC mnamo Februari 2024.
“Rais hatakuwa akitangazia tu Wakenya, bali pia Afrika na jamii ya kimataifa kuwa mwaniaji wa Kenya katika kinyang’anyiro cha AUC ni Raila Amolo Odinga,” akasema Kinara wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi kuelekea hafla ya kesho.
Katika hafla hiyo, Rais anatarajiwa pia kuzindua sekretariati ambayo itasimamia kampeni za Bw Odinga ambazo zinatarajiwa kutafadhiliwa na serikali.
Japo Raila alikuwa amebuni sekretariati yake, inatarajiwa itaunganishwa na wanamikakati kutoka serikali ambao majina yao yatatangazwa na Rais Ruto.
Pia, mtandao ambao unamsawiri Raila kama anayetosha kutwaa wadhifa huo utazinduliwa ili kuimarisha nafasi yake ya kupata ushindi.
Kulingana na Bw Mudavadi, kampeni za Raila zitaendeshwa na watu wenye ujuzi mkubwa na hekima nyingi ambao wataandamana naye katika nchi mbalimbali.
“Kampeni ya Raila haitakuwa ya mzaha kwa sababu tutatumia nguvu na jitihada zote baada tu ya uzinduzi wa Jumanne kukamilika. Wizara ya Kigeni ambapo mimi ndio nasimamia itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Kenya inapata kiti hiki,” akaongeza Bw Mudavadi.
Wapinzani wa Bw Odinga katika kiti cha AUC ni Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Mahmoud Youssouf, Anil Kumarsingh Gayan ambaye ni waziri wa zamani wa nje wa Mauritius na mwenzake wa zamani wa Kisiwa cha Madagascar Richard James Randriamandrato.
Kuondoka kwa Raila katika siasa za Kenya tayari kumepisha mivutano ndani ya ODM huku Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino wakipigania kumrithi chamani.