Raila kuomba kura moja kwa moja kwa marais wa Afrika walioko China
WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga anatarajiwa kunadi azma yake ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) moja kwa moja mbele ya marais wa Afrika jijini Beijing, China siku chache baada ya kuzinduliwa rasmi na serikali.
Bw Odinga aliandamana na Rais William Ruto katika Mkutano wa Tisa kuhusu Ushirikiano Kati ya China na Afrika (FOCAC) unaoanza Jumatano, Septemba 4, 2024 ambapo anatarajiwa kutoa hotuba kuhusu miundo msingi.
Waziri huyo Mkuu wa zamani aliwahi kuhudumu kama Mwakilishi wa Umoja wa Afrika kuhusu Ustawi wa Miundo Msingi Afrika kati ya 2018 na 2023.
Mkuu wa Sekritariati ya kuendesha kampeni za Bw Odinga, Dkt Korir Sing’oei aliambia Taifa Dijitali kwamba Waziri huyo Mkuu wa zamani yuko China kama “mshirika muhimu wa Afrika kuhusu miundo msingi.”
“Mwaniaji huyo wa uenyekiti wa AUC atakutana na viongozi mbalimbali kubadilishana mawazo kuhusu miundo msingi, muktadha wa mpango wa ujenzi wa barabara, nguzo kuu katika ushirikiano kati ya China na Afrika,” akaeleza Dkt Sing’oei, ambaye ni Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni.
Mkuu wa Mawaziri ambaye pia anahudhuria mkutano huo, bw Musalia Mudavadi, alisema Rais Ruto atafanya mashauriano na Rais wa China Xi Jinping, pamoja na marais wengine wa mataifa ya Afrika kupalilia ushirikiano kati yao na Kenya.
Mazungumzo kati ya Dkt Ruto na Bw Jinping yaliangazia ushirikiano kati ya Kenya na China katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
“Atafanya mashauriano na marais na viongozi wa serikali kutoka nchi mbalimbali za Afrika kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Aidha, atatumia nafasi hiyo kumnadi Bw Odinga kama mgombeaji bora wa wadhifa wa mwenyekiti wa AUC,” akaeleza Bw Mudavadi.
Aliyekuwa balozi wa Kenya Amerika Elkana Odembo, ambaye pamoja na Dkt Sing’oei wanaongoza sekritariati ya kushirikisha kampeni za Bw Odinga, alisema mkutano wa FOCAC unaohudhuriwa na marais wa Afrika unampa mgombeaji huyo nafasi bora ya kuzungumza na viongozi hao pembezoni mwa kumbi za mikutano.
“Kimsingi, Bw Odinga anahudhuria mkutano wa FOCAC jijini Beijing kama mshirika mkuu kutoka Afrika. Aidha, atatumia jukwaa hilo kuomba kura moja kwa moja kutoka kwa marais wa Afrika. Marais hao ndio watakaoshiriki upigaji kura kuchagua mwenyekiti mpya wa AUC Februari mwaka ujao, 2024,” Bw Odembo akaambia Taifa Dijitali.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga