Rais kigeugeu? Wanawake, vijana Lamu walia kutengwa Ruto akiteua makatibu
VIJANA na akina mama katika Kaunti ya Lamu wamemkosoa Rais William Ruto kwa kutotimiza ahadi yake ya kuwajumuisha katika serikali yake.
Kauli yao inatokana na kuteuliwa kwa makatibu 14 wa wizara mbalimbali mnamo Alhamisi juma hili (Machi 20, 2025).
Vijana na akina mama hao wanasikitika kwamba hakuna mlalahoi au mtu yeyote wa tabaka la chini aliyeteuliwa serikalini.
Afisa Mtendaji wa Muungano wa Wanawake Lamu, Women Alliance (LAWA), Bi Raya Famau alisema uteuzi uliotangazwa na Rais Ruto Alhamisi ulidhihirisha wazi kwamba azma yake ni kujipanga jinsi atakavyoshinda uchaguzi mkuu wa 2027 na wala si kuzingatia ahadi zake, ikiwemo kuhakikisha serikali yake ni ya kuwajali na kuwajumuisha walalahoi.
Alishikilia kuwa kila anaposimama jukwaani, Rais Ruto amekuwa akidai serikali yake ni ya watu wa matabaka yote na kwamba walalahoi ndio watakaojumuishwa.
Bi Famau hata hivyo alimkosoa Rais Ruto, akimtaja kiongozi anayethamini ukabila, siasa na tabaka la juu ili kujinufaisha mwenyewe wala si kusaidia watu wa chini kama anavyodai kwenye hotuba zake.
“Kwa nini Wakenya tuchezewe namna hii? Kila wakati Rais Ruto akisimama anasema serikali ni ya walala hoi. Kati ya makatibu wote 14 alioteua Alhamisi, mlalahoi ni yupi hapo. Sijaona mama mboga au msukuma rukwama hapo. Uteuzi umefuata tabaka la juu, mirengo na vyama vya kisiasa, ukabila, urafiki na mengineyo. Yaani yote hayo ni kujipanga tu kuangalia jinsi watashinda siasa za 2027. Tumechoka kuchezewa,” akasema Bi Famau.
Ahmed Ali, mmoja wa vijana Lamu, alieleza kushangazwa kwake na jinsi maeneo kama vile Lamu na ukanda wa Pwani umeendelea kutelekezwa kiuongozi, hasa katika ngazi za kitaifa.
Bw Ali alisema kwenye uteuzi wa makatibu wa wizara mbalimbali Alhamisi, katu hakuona mtu yeyote wa Lamu akiteuliwa.
“Lamu tumezoea kutelekezwa kisiasa na uongozi. Ilianza zamani tangu uhuru wa nchi hii kupatikana. Baada ya kumteua katibu mmoja wa Wizara, ambaye ni Bw Abubakar Hassan, Lamu imeonekana tayari kutosheka kwa hilo. Nilitarajia kwamba tungeongezewa nafasi ya makatibu kwenye listi ya Alhamisi. Sijafurahia kama kijana,” akasema Bw Ali.
Bi Husna Bakari naye alisema matarajio yake ilikuwa ni kuona tabaka la chini na jinsia ya kike, hasa kutoka Lamu wakiteuliwa kama makatibu wa wizara.
“Tulikuwa na katibu wa Wizara ya Ujenzi kutoka Lamu ambaye ni Bi Maryam El Maawy. Baada ya kifo chake 2017, tumekuwa tukiimba nafasi yake ipatiwe mwanamke kutoka Lamu. Wasomi wapo na tunaweza. Kwa nini Rais Ruto hangezingatia hilo kwenye listi? Hatufurahii,” akasema Bi Bakari.