Ripoti yafichua jinsi bangi inavyoingizwa Kenya kirahisi bila matatizo
LICHA ya vita vinavyoendelea vya kutokomeza ulanguzi wa bangi, imebainika kuwa kuna njia 22 ambazo zinatumika kuingiza dawa hiyo ya kulevya nchini.
Njia hizo zipo kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia, Tanzania na Uganda. Ethiopia ndiyo inaongoza kwenye orodha hiyo kwa kwani ina njia 11 ambazo zinatumika kuingiza bangi Kenya.
Uganda na Tanzania zina njia saba na nne mtawalia. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ambayo imetolewa na Kituo cha Kitaifa cha Utafiti Kuhusu Uhalifu (NCRC).
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa bangi hupakiwa kisha kufichwa na kufunikwa vizuri ili kuzuia maafisa wa polisi kugundua. Maeneo ya Mashariki, Magharibi, Kati, Nyanza na Kati huwa na miundombinu bora ambayo husaidia kurahisisha kusafirishwa kwa bangi.
Ilibainika bangi hiyo hasa hupelekekwa Nairobi na Mombasa huku ikibainika kuwa biashara hiyo huwa imeenea sana jijini Nairobi ambapo bangi huingizwa kwa zaidi ya njia 17 tofauti.
Mombasa inafuata kwa kuwa na njia 13 tofauti ambazo bangi huingizwa humo. Utafiti huo unasema kuwa njia rahisi za kuingiza bangi Kenya kutoka Ethiopia huwa ni Moyale.
Mji huo ambao upo Kaskazini mwa Kenya unatumika kuingiza bangi kutoka Ethiopia maarufu kama Shash. Barabara ambazo zinatumika ni Ethiopia-Moyale-Mandera-Garissa hadi Mombasa.
Kutoka Moyale, bangi hiyo husafirishwa hadi Marsabit kisha Isiolo na hupelekwa Meru au Nairobi. Pia kuna njia ya Ethiopia-Moyale-Garissa-Thika-Nakuru/ Mombasa.
Ili kusambaza bangi hiyo vizuri, walanguzi wamekuwa wakihiari kutumia njia ya Marsabit kwa sababu inawawezesha kufikisha bangi kwa rahisi hadi Mandera, Garissa kisha Nairobi hadi Mombasa.
Wakati ambapo kuna hitaji la dharura na bangi inahitajika sana, ripoti ya NCRC inasema walanguzi hutumia njia ya Ethiopia-Moyale-Mandera-Garissa-Thika-Nairobi.
Kando na Nairobi na Mombasa, Marsabit pia hurahisisha bangi kufika Ziwa Turkana, Lodwar na Kitale. Njia nyingine ni Ethiopia-Forole ambapo bangi husafirishwa kiharamu hadi miji ya Kargi, Wamba, Marlan, Nyahururu kisha Nairobi.
Bangi kutoka Tanzania nayo huingizwa kupitia Migori ambayo ni kati ya njia sita zinazotumika. Bangi hiyo inayofahamika kama ‘Bongo’ pia huingizwa kupitia Muhuru Bay.
Barabara za Tanzania-Migori-Kisii-Narok-Ntulele-Mai Mahiu-Naivasha-Nairobi/Mombasa na pia Tanzania-Migori-Oyugis-Kisumu-Eldoret hutumika kufikisha bangi hiyo Nairobi na Mombasa.
Bangi ya Uganda inayofahamika kama banange huingia Kenya kupitia miji ya mpaka ya Busia na Malaba. Mji wa Sio Port kwenye Ziwa Viktoria pia hutumika kuingiza bangi hiyo Kisumu, Kericho, Nakuru, Nairobi na Mombasa.
Kwa mujibu wa NCRC, njia hizo hubadilika kila mara kwa sababu walanguzi wana mtandao wa watu ambao huchunguza na kufuatilia iwapo ni salama kupitisha dawa hiyo ya kulevya.
Watu hao wanalipwa hela nyingi kueleza jinsi hali ilivyo barabarani na iwapo kuna hatari ya kunyakwa na maafisa wa usalama
“Mipaka ambayo haina doria ya kutosha, hitaji la juu na soko imara pamoja na utajiri wa haraka ndiyo hurahisisha kuingizwa kwa bangi nchini,”ikaongeza ripoti hiyo ya NCRC.