Ruto acheza pata potea akipanga tena mawaziri
HATUA ya Rais William Ruto kufanyia mabadilikko baraza lake la mawaziri mara ya tatu katika muda wa chini ya miaka mitatu, ambapo alimpiga kalamu Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi inamsawiri kama anayebahatisha kufanya serikali yake kufanikiwa.
Kinachovutia zaidi ni jinsi anavyohamisha baadhi ya mawaziri kutoka wizara moja hadi nyingine bila kuzingatia taaluma na tajiriba yao katika wizara husika.
Mbali na kumteua Mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku kujaza nafasi yake Bw Muturi katika wizara ya Utumishi wa Umma, labda kutuliza wakazi wa Kaunti ya Embu anakotoka spika huyo wa zamani wa Bunge la Kitaifa, Rais Ruto alimhamisha Aden Duale kutoka Wizara ya Mazingira hadi Wizara ya Afya ambayo ilikuwa imeshikiliwa na Dkt Debora Barasa ambaye licha ya kuwa mtaalamu wa masuala ya afya atasimamia Wizara ya Mazingira.
Duale, ambaye alikuwa mwalimu kabla ya kujiunga na siasa, atahudumu katika wizara ya tatu chini ya utawala wa miaka miwili na nusu wa Kenya Kwanza ambao Rais amebadilisha baraza lake la mawaziri mara tatu.
Kwenye taarifa iliyotolewa Jumatano, Machi 26, 2025 na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, kiongozi wa taifa pia alimteua Bi Hanna Wendot Cheptumo kuwa Waziri wa Masuala ya Jinsia na Utamaduni.
Bi Cheptumo ni mjane wa aliyekuwa seneta wa Baringo marehemu William Cheptumo.
“Wawili hao wanatarajiwa kuleta katika baraza la mawaziri sio tu uelewa na maarifa ambayo wamepata katika taaluma zao kwa kipindi kirefu, bali hekima waliopata katika safari zao maishani,” ilisema taarifa iliyotangaza mabadiliko ya Jumatano.
Majina ya Bi Cheptumo na Bw Ruku sasa yatawasilishwa bungeni kupigwa msasa kubaini ufaafu wao kwa nyadhifa hizo muhimu, bunge la kitaifa litakaporejelea vikao vyake Aprili 2, 2025 baada ya likizo fupi.
Wakati huo huo, Rais Ruto pia amewabadilisha mawaziri wawili, Aden Duale (Mazingira) na Deborah Barasa (Afya).
Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/sababu-za-ruto-kumfuta-kazi-justin-muturi/
Bw Duale sasa atahudumu kama Waziri wa Afya huku Dkt Barasa akihudumu kama Waziri wa Mazingira.
Duale anajiunga na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kama mawaziri ambao wameshikilia wizara nyingi zaidi katika utawala chini ya miaka mitatu wa Rais Ruto huku baadhi ya mawaziri wakihamishwa au kufutwa kazi baada ya kuhudumu kwa chini ya miezi sita.
Wizara ya kwanza ya Murkomen kusimamia chini ya utawala wa Rais Ruto ilikuwa ya Uchukuzi, kabla ya kuteuliwa waziri wa Vijana na Michezo mwaka jana, 2024, Rais alipounda upya baraza lake la mawaziri alilovunja kufuatia maandamano ya vijana, Gen Z.
Ili kupisha serikali Jumuishi kufuatia ukuruba wake na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Rais Ruto aliwafuta kazi mawaziri wawili waliohudumu kwa chini ya miezi sita.
Dkt Margaret Ndungu, mtalaam wa mawasiliano aliyekuwa waziri wa ICT na Uchumi Dijitali aliteuliwa balozi wa Kenya nchini Ghana wadhifa aliokataa huku nafasi yake ikitwaliwa na aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo.
Dkt Andrew Karanja aliyekuwa Waziri wa Kilimo aliteuliwa balozi wa Kenya nchini Brazil ambao alikubali.
Nafasi yake katika wizara ya Kilimo ilichukuliwa na Bw Mutahi Kagwe ambaye ni mtaalamu wa mawasiliano na ambaye alisimamia Wizara ya Afya katika utawala wa Jubilee.
Rais Ruto pia amewashirikisha wanachama watano wa ODM katika serikali yake wanaosimamia wizara muhimu ambazo zinapaswa kushikiliwa na wandani wake katika Kenya Kwanza.
John Mbadi aliyekuwa mwenyekiti wa ODM ni Waziri wa Fedha, Opiyo Wandayi ni Waziri wa Kawi, Hassan Joho anasimamia madini na Wycliffe Oparanya anasimamia Ushirika huku Beatrice Askul akiongoza Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wachambuzi wa siasa na utawala wanasema kwamba anachofanya Rais Ruto ni kujikita kisiasa, kuepuka changamoto zozote anazohisi na kutia mizizi utawala wake akilenga kutimiza ajenda zake za maendeleo na siasa.
“Rais Ruto anakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo uasi wa zilizokuwa ngome zake na kutotimiza ahadi za uchaguzi. Ana kibarua cha kusawazisha maslahi ya kisiasa huku akitekeleza ajenda ya maendeleo wakati ambao umaarufu wake unashuka. Zaidi anajali maslahi ya kisiasa kuelekea 2027,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Musili Koli.