Ruto anavyompiga kumbo Kalonzo kujimegea wafuasi wa Raila
ZIARA ya Rais William Ruto katika eneo la Nyanza katika Kaunti ya Kisumu, imeonekana kuyeyusha kabisa matumaini ya Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka wa kurithi ngome hiyo ya Kinara wa ODM Raila Odinga.
Ukuruba kati ya Rais na Bw Odinga umenoga mno, hasa baada ya wandani wa waziri huyo mkuu wa zamani kuchaguliwa ndani ya utawala wa sasa mwezi uliopita.
Rais Jumanne wiki jana alizindua rasmi kampeni za Bw Odinga za kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ambapo alisema kuwa serikali itaendesha kampeni kali kuhakikisha kuwa kiongozi huyo wa upinzani anachukua wadhifa huo.
Tangu kuanza kwa ukuruba wa Rais na Raila, Bw Musyoka ameonekana kuwa na wazo tofauti, akimshambulia Bw Odinga na hata kujitangaza kama kiongozi wa upinzani nchini.
Bw Musyoka hasa alishutumu Raila kwa usaliti baada ya vigogo wanne wa ODM kuchaguliwa mawaziri, hatua aliyosema ilikuwa ya kukinga serikali ya Ruto iliyokuwa ikiporomoka wakati wa maandamano ya Gen Z mwezi uliopita.
Mnamo Ijumaa, Rais Ruto alionekana kuashiria kuwa analenga kuweka kura za Nyanza katika kapu lake aliposema kuwa hawezi kukubali eneo hilo lisalie upinzani milele hata Bw Odinga akifanikiwa AUC.
Kiongozi wa nchi alisema kuwa wakati ulikuwa umefika ambapo mwenge wa upinzani nao unastahili kubebwa na maeneo mengine kwa sababu haukutengewa Nyanza pekee.
“Nimeongea na Kiongozi wa Wachache kwenye Bunge la Kitaifa Junet Mohamed na tumezungumzia uwezekano wa kuacha nafasi hii ya upinzani uende kwingine baada ya miaka mitatu,” akasema Rais huku akishangiliwa na umati.
Rais alikuwa akiongea Sindindi eneobunge la Ugunja wakati wa siku ya tatu ya ziara yake Nyanza.
Hafla ya Wandayi
Alikuwa akihudhuria hafla ya kumkaribisha nyumbani Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi baada ya kufungua miradi ya maendeleo maeneobunge ya Bondo na Alego Usonga.
“Au mnataka tuendelee na upinzani. Si kama kuna wengine wanatafuta tuwapatie pia,”akaongeza Rais akionekana kusisimua mno umati mkubwa ambao ulikuwa umejitokeza kumkaribisha.
Matamshi hayo yanaonekana kulenga viongozi wengine wa Azimio ambao wanaonekana kumvamia Raila mara kwa mara baada ya kuwaasi na kukumbatia serikali.
Bw Musyoka, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Kinara wa Narc Kenya Martha Karua na kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa hawakuhudhuria hafla ya kuzindua azma ya Bw Odinga ya kuwania uenyekiti wa AUC katika ikulu Jumanne.
Mapokezi ambayo Rais alipata katika kaunti za Migori, Homa Bay, Siaya na Kisumu pamoja na kauli za wandani wa Raila, yalikuwa ishara tosha kuwa eneo hilo linaelekea kwenye kambi ya Ruto mnamo 2027.
Hii ni licha ya kuwa Kalonzo ameunga mkono Raila kwenye chaguzi za 2013, 2017 na 2022.
“Ningependa kuwaambia baadhi ya viongozi wanaofikiria kuwa kuna sababu zilizofanya nifanye kazi na Raila. Hakuna la mno na tuliamua tu kuzika tofauti zetu za kisiasa
“Ushindi nilioupata mnamo 2022 haukuwa wangu pekee bali pia wa watu wa Nyanza ambao hawakunipigia kura,” akaongeza Rais.
Kuonyesha kuwa huenda viongozi wa ODM wamemzika Bw Musyoka kwenye kaburi la sahau, waliohutubu walimwaambia Rais Ruto kuwa wapo tayari kumuunga mkono kisiasa iwapo ataendelea kushirikiana na kigogo wao wa kisiasa.
Kinyume na hapo awali ambapo Rais alipata wakati mgumu kisiasa Nyanza, aliandamana na viongozi wote waliochaguliwa maeneo alikofika huku wananchi wakimshabikia.
Mlima umemponyoka
Rais anaonekana kulenga ngome za Raila baada ya uungwaji mkono wake kuonekana kuwa vuguvugu eneo la Mlima Kenya ambapo anatoka naibu wake Rigathi Gachagua.
Wawili hao wamekuwa na ushindani wa chini kwa chini kisiasa huku wanasiasa wa mlimani wakiweka bayana kuwa hawajafurahishwa na kujumuishwa kwa wandani wa Raila serikalini.
Ijumaa, Bw Musyoka akiwa Pwani alisema kuwa anaunga azma ya Raila ya AUC lakini haungi mkono ushirikiano wake na Rais Ruto huku akisema anaendelea na maandalizi yake ya kuwania urais 2027.