Habari za Kitaifa

Ruto aondoka nchini bila naibu rais, aagwa na wakuu wa usalama

Na BENSON MATHEKA October 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KWA mara ya kwanza tangu kuondolewa ofisini kwa naibu wake Rigathi Gachagua, Rais William Ruto ameondoka nchini kuhudhuria mkutano wa 23 wa wakuu wa nchi na serikali wa Shirika la Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) mjini Bujumbura, Burundi.

Rais Ruto aliagwa katika uwanja wa ndege na maafisa wakuu wa usalama wakiongozwa na katibu wa usalama wa ndani Dkt Raymond Omollo, Mkuu wa Majeshi Jenerali Charles Muriu Kahariri na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed katika taarifa alisema kiongozi wa nchi aliondoka mapema Alhamisi kwa mkutano ambao unaadhimisha miaka 30 ya Comesa.

Comesa ni shirika muhimu la kibiashara la soko la pamoja la watu milioni 640 na inawakilisha soko kubwa la Kenya, ambalo kwa sasa linashikilia asilimia 12.4 ya soko la kikanda, ikiwa ya  pili baada ya Misri.

Ikulu ilisema kuwa kati ya 2019 na 2023, mauzo ya Kenya kwa COMESA yalikua kwa asilimia 8.9, ikiangazia uwezekano mkubwa wa biashara na ushirikiano wa kikanda.

“Katika ziara yake, Rais atashiriki mijadala ya hali ya juu yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa Kenya na washirika wakuu wa kimkakati, kwa kuzingatia hasa kuimarisha mfumo wa thamani ya kikanda ili kuimarisha ushirikiano wa Comesa,” Bw Mohamed alisema.

Rais pia ameratibiwa kukutana na Marais wa Misri na Zambia, pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia, miongoni mwa wengine.

Majadiliano na Misri yatalenga katika kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Misri huku mkutano na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ukinuia  kuwezesha biashara.

Rais Ruto pia atachukua fursa hiyo kupigia debe mwaniaji wa Kenya wa wadhifa wa mwenyekiti Tume ya Muungano wa Afrika Raila Odinga.

Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni Dkt Korir Sing’oei alisema Bw Odinga ambaye alikuwa ameratibiwa kuhudhuria mkutano huo hata hivyo hatakuwepo.