Ruto aponda Kalonzo, akimwaga minofu Ukambani
Rais William Ruto amewataka wakazi wa Ukambani kumwacha kiongozi wa Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, na kuunga mkono azma yake ya kuchaguliwa tena mwaka 2027.
Rais alisema serikali yake inalenga kuleta maendeleo katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni, akidai upinzani hauna mpango madhubuti wa kubadilisha maisha ya wakazi.
Akizungumza katika mikutano mbalimbali baada ya kuzindua na kukagua miradi ya barabara, maji, nyumba na umeme vijijini, Ruto alisema Ukambani umekuwa nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi.
“Hatutaki Ukambani iendelee kubaki nyuma. Tunaunganisha Wakenya wote kupitia serikali jumuishi itakayojumuisha watu wa eneo hili,” alisema akiwa Mbiuni, Kaunti ya Machakos.
Alionya wakazi dhidi ya viongozi wanaotumia siasa za kikabila na ubaguzi, akisema Wakenya wote ni ndugu na wanafaa kushirikiana kuleta maendeleo.
Katika mikutano hiyo, alimkosoa kwa kushindwa kuboresha barabara inayoelekea nyumbani kwake licha ya kuhudumu katika nyadhifa za juu serikalini kwa miaka mingi.
Hata hivyo, Ruto alilaumu tawala zilizopita kwa kupuuza eneo hilo katika mipango ya maendeleo, akiahidi kurekebisha hali hiyo.
Ujenzi wa barabara ya Kandwia-Kyuso-Tseikuru unatarajiwa kuanza Jumatatu, siku ambayo rais anatarajiwa kuzindua ujenzi wa mabweni katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Tseikuru.
Miradi hiyo ni sehemu ya mipango ya miundombinu ya thamani ya zaidi ya Sh150 bilioni iliyotengewa kaunti hizo tatu.
Katika Makueni, rais alizindua barabara ya Wote-Kako-Ngoluni na Kyambeke-Kyuasini-Ukia, huku akizindua rasmi barabara iliyokamilika ya Tawa-Itangini.
Katika Kaunti ya Kitui, alizindua ujenzi wa barabara ya Kwa Vonza-Kanyangi-Kyandula.
Ruto alisema serikali imetenga Sh21 bilioni kuweka lami barabara mpya 10 Machakos na Sh16 bilioni kwa barabara saba Makueni.
Aidha, alisema Sh28 bilioni zimetengwa katika mwaka wa kifedha wa 2026/2027 kujenga nyumba 8,000 za gharama nafuu, mabweni 6,000 na masoko 18 Machakos.
Katika Mbiuni, alizindua mradi wa maji wa Mwala Cluster wa thamani ya Sh1.47 bilioni, unaolenga kusambaza lita milioni 6.6 za maji kila siku kwa wakazi wa maeneo ya Kangundo na Mwala.
Ziara hiyo pia ilishuhudia Mbunge wa Yatta, Robert Basil, akihama Wiper ya Kalonzo na kujiunga na UDA ya Ruto. Basil alimtaja rais kuwa mkombozi wa jamii ya Wakamba, huku Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka, akihimiza wakazi kumuunga mkono katika uchaguzi ujao.
Leo, Ruto anatarajiwa kuhudhuria ibada katika Kanisa la AIC Kasina, Mwingi ya Kati, kabla ya kukagua ujenzi wa Daraja la Mto Enziu.
Daraja hilo limekuwa suala muhimu tangu Desemba 2021, basi lililokuwa limebeba waumini wa Kanisa Katoliki kwenda harusi liliposombwa na maji na kusababisha vifo vya watu 31. Ruto amesema serikali yake imejitolea kukamilisha mradi huo.