Habari za Kitaifa

Ruto atetea uamuzi wa serikali yake kuajiri walimu vibarua

Na RUSHDIE OUDIA August 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto alitetea uamuzi wa serikali yake kuwaajiri walimu kama vibarua badala ya mkataba wa kudumu, akisema hatua hiyo itapunguza kero la uhaba wa walimu katika shule za umma.

Kiongozi wa taifa alieleza kuwa hatua hiyo imemsaidia kuua ndege wawili kwa jiwe moja kwa kuhakikisha kuwa walimu waliosalia bila ajira kwa miaka mingi wamepata kazi na wanafunzi wanasomeshwa.

Kulingana na Dkt Ruto, taifa linakumbwa na uhaba wa 140,000 na kuna jumla ya walimu 300,000 waliohitimu.

Baadhi yao wanaelekea kustaafu kabla ya kuajiriwa na Tume ya Huduma za Walimu (TSC).

“Kama ningeamua kuajiri walimu kwa mkataba wa kudumu, ningeajiri walimu 13,000 pekee. Kwa hivyo, niliamua kuchukua idadi kubwa ya walimu wasio na ajira na kuwaajiri kama vibarua. Kwa njia hiyo, nilisuluhisha matatizo mawili, kwani nitamwezesha mtu ambaye hakuwa anapata chochote au Sh5, 000 na sasa watapata angalau 25, 000. Vile vile, mwanafunzi ambaye hakuwa na mwalimu sasa amepata mwalimu,” akasema Dkt Ruto.

Alieleza kuwa baada ya walimu hao kuhudumu kwa miaka miwili, vibarua hao watapewa ajira ya kudumu.

Kundi la kwanza la walimu vibarua waliajiriwa Januari mwaka jana na muda wa kandarasi yao uliongezwa kwa mwaka mmoja mwanzoni mwa mwaka huu, 2024.

Siku chache zilizopita, Waziri wa Elimu Julius Migos alisema serikali imetenga Sh18.7 bilioni kufadhili mpango wa kuwaajiri kwa mkataba wa kudumu walimu 46,000 wanaofundisha katika Shule za Upili za Msingi (JSS).

Alisema kuwa walimu hao wataajiri kuanzia Januari 2025. Walimu hao wa JSS waligoma mnamo Mei na Juni wakishinikiza waajiriwe kwa mkataba wa kudumu.

Rais Ruto alikuwa akiongea katika kikao cha hadhara jijini Kisumu Alhamisi usiku ambapo alivishutumu vyama vya kutetea masilahi ya walimu kuwachochea walimu kugoma licha ya serikali kutimiza matakwa yao.

Alisema kuwa serikali itatimiza yale yote yaliyoko katika mkataba wa maelewano (CBA) na kwamba watalipwa malimbikizi ya nyongeza ya mishahara.

Serikali ilitoa Sh13.7 bilioni kugharamia nyongeza hiyo ya mishahara.

“Kwa hivyo, hamna sababu ya mtu kuwaambia walimu wagome. Ningependa kupongeza Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kwa kuelewa kuwa tunaendelea kutekeleza matakwa yao. Wamefutilia mbali mgomo ili kuwawezesha watoto wetu wasome,” Dkt Ruto akasema.