Habari za Kitaifa

Ruto atuma Raila Sudan Kusini kupatanisha viongozi

Na BENSON MATHEKA,MASHIRIKA March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amemtuma  aliyekuwa  waziri mkuu Raila Odinga kwenda Sudan Kusini kama mjumbe maalum kusaidia kupunguza mvutano unaozidi kutokota kati ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake wa muda mrefu, Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, hali inayotishia kurudisha nchi hiyo vitani.

Machar amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani katika mji mkuu wa Juba tangu Jumatano usiku, chama chake kimesema, jambo ambalo kimsingi linavunja makubaliano ya amani ya 2018 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano na kuwaleta viongozi hao wawili katika serikali dhaifu ya kugawana madaraka.

Chama cha Machar SPLM- IO, kimekana madai ya serikali kwamba kinaunga mkono Jeshi Jeupe, kundi la wanamgambo wa kikabila linaloundwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa jamii ya Nuer, ambalo lilipambana na jeshi katika mji wa kaskazini-mashariki wa Nasir mwezi huu, na hivyo kuchochea mzozo wa kisiasa uliopo sasa.

Kufuatia mapigano hayo, vikosi vya Kiir vilikamata washirika wa karibu wa Machar, akiwemo waziri wa mafuta na naibu mkuu wa jeshi.

Vikosi vinavyomtii Kiir na Machar vimepigana katika siku za hivi karibuni, nje ya Juba na maeneo mengine.

Rais wa Kenya William Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Alhamisi alisema ameongea na Kiir kuhusu kifungo cha Machar na anamtuma mjumbe maalum kusaidia kupunguza mvutano huo na kutoa ripoti ya hali ilivyo.

Msemaji wa Odinga, Dennis Onyango, alithibitisha kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani alitarajiwa kusafiri kwenda Juba Ijumaa.

Ruto alisema pia amewasiliana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ambaye mwezi huu alituma wanajeshi kwenda Sudan Kusini kwa ombi la serikali ili kusaidia kulinda mji mkuu, pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye hapo awali ameandaa mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini.

Makundi hasimu yanayomuunga mkono Kiir na Machar yalipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 2013 hadi 2018, vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu.