Habari za Kitaifa

Ruto: Hakuna mtu alitekwa nyara katika maandamano

Na RUSHDIE OUDIA August 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amesema hakuna utekaji nyara uliotekelezwa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano ya kupinga serikali.

Alisema haya huku baadhi ya familia zikiendelea kuwasaka jamaa zao miezi kadhaa baada ya kutoweka kwa namna ya kutatanisha kufuatia maandamano.

Kuna baadhi ya visa vilivyoripotiwa ambapo watu fulani “walitekwa nyara” mchana peupe na maafisa waliojihami wakiwa wamevalia kiraia.

Akijibu maswali katika Baraza la Jiji, Dkt Ruto alisema anazingatia ahadi aliyotoa alipochukua usukani ya serikali kuwa hatatumia polisi kuwateka nyara na kuwaua Wakenya wasio na hatia.

Rais alisema hana habari kuhusu utekaji nyara wowote, akizitaka familia ambazo jamaa wao wametoweka kuwasilisha majina yao kwa serikali ili hatua ichukuliwe.

“Chini ya usimamizi wangu, sitaki hali ambapo Wakenya wanatoweka. Kuna siku watu zaidi ya 20 walikuwa wanapatikana Mto Yala hapa wakiwa wameuawa. Nataka kuwaahidi haya hayatatendeka chini ya uangalizi wangu,” alisema Dkt Ruto.

Rais aliagiza familia kupeleka majina kwa Katibu wa Wizara ya Usalama, Raymond Omollo, aliyekuwepo vilevile katika kikao hicho.

“Familia yoyote ambayo mtu au jamaa wao alienda katika maandamano iwe mwaka jana au mwaka huu na hakurejea, nataka kujua majina yao ili nichukue hatua madhubuti, kwa sababu ninapozungumza nanyi leo, sina jina la mtu aliyetekwa nyara au kutoweka.”

Alipoulizwa atakachofanya kufidia wahasiriwa wa maandamano, Dkt Ruto alisema serikali inabuni mfumo wa kusaidia familia zilizoathiriwa.

“Tunafuatilia idadi ili kubaini ni vipi (wahasiriwa) watashughulikiwa.”

Kisumu ni miongoni mwa kaunti ambazo zimekuwa zikiathiriwa zaidi na ghasia na ukatili wa polisi unaosababisha majeraha na vifo.

Rais aliwasuta raia kwa kushiriki ufisadi pamoja na polisi akiwahimiza wasitoe rushwa kwa maafisa ili wasaidiwe katika masuala mbalimbali.

“Tutakabiliana na ufisadi lakini Wakenya ni sharti wakomeshe mtindo wa kuwapa hongo polisi kwa sababu maafisa hawawezi kuzuia vita dhidi ya ulaji rushwa. Tutawachukulia hatua wahusika wote wawili,” alifoka.

Alisema kuna mipango ya kuhamisha mifumo ya kidijitali katika vituo vyote vya polisi ili kuhakikisha taarifa zote zinazoandikishwa kwenye kitabu cha matukio (OB) zinahifadhiwa na kupunguza visa vya kurasa za OB kutoweka.