Habari za Kitaifa

Ruto sasa apeleka mawaziri mbio, ataka watimize ahadi ndani ya mwaka mmoja

Na MOSES NYAMORI September 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amewapa malengo mapya ambayo ni magumu mawaziri wake ambayo anataka watimize ndani ya mwaka mmoja.

Malengo hayo ni sehemu ya harakati za hivi punde za Rais Ruto kutimiza ahadi nyingi alizotoa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022, ambazo nyingi zao hazijatimizwa miaka miwili tangu aingie mamlakani.

Pia, yamkini ni kama jibu kwa vijana walioandamana kulalamikia utendakazi duni wa Baraza la Mawaziri lililovunjwa.

Mawaziri wote wamepewa mwaka mmoja ili kutekeleza miradi maalum yenye umuhimu chini ya nguzo tano za Kilimo, huduma ya afya kwa wote, uchumi wa kidijitali, mikopo nafuu pamoja na utengenezaji na uongezaji thamani.

Mawaziri wengi na Makatibu sasa wamejitolea kutimiza malengo mahususi katika kandarasi za utendakazi.

Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri na Wizara ya Mashauri ya Nje na Masuala ya Wakenya wanaoishi ng’ambo chini ya Bw Musalia Mudavadi, Waziri Eric Muuga (Maji, Usafi wa Mazingira na Unyunyuzaji), Andrew Karanja (Kilimo), Wycliffe Oparanya (Ushirika), Alice Wahome (Ardhi) na Salim Mvurya (Uwekezaji na Biashara) ni baadhi ya Mawaziri ambao wamejadiliana na kuidhinisha miradi itakayokamilishwa ndani ya muda uliowekwa.

Zoezi hilo linasimamiwa na Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi Kuu ya Rais anayohusika na Utendakazi na Usimamizi wa Utekelezaji serikalini, Bw Eliud Owalo, na Katibu wa Baraza la Mawaziri Bi Mercy Wanjau.

Waziri Muuga ameagizwa kuongeza unyunyuziaji maji mashamba hadi ekari 773,069 za ardhi. Wizara inapanga kuwa na ekari 40,000 za ziada chini ya unyunyuziaji ifikapo Juni mwaka ujao.

Wizara pia inapanga kuongeza uzalishaji wa mpunga hadi tani 250,000. Hii, waziri anasema, itazalisha jumla ya mazao ya thamani ya Sh23 bilioni na kuziba nakisi ya mpunga.

Katika malengo yake, wizara ya Mudavadi, ilisema itaongeza pesa ambazo Wakenya wanaoishi nje ya nchi wanatuma nchini kutoka Sh400 bilioni mnamo 2022 hadi Sh607 bilioni mnamo 2024 huku ikijitolea kuimarisha ushirikiano wa Wakenya wanaoishi ughaibuni kupitia Mkakati wa Uwekezaji.

Waziri Wahome aliahidi kuhakikisha kuwa wizara yake itajenga nyumba 66,155 za bei nafuu hadi viwango mbalimbali na nyumba za makazi za kijamii 52,758 hadi viwango mbalimbali vya kukamilika ifikapo Juni.

Wizara pia inajitolea kujenga nyumba 41,964 zinazojumuisha 24,152 za Polisi wa Kitaifa, 10,033 za Jeshi la Ulinzi la Kenya na 7,779 za makazi ya Wanafunzi.

Pia, katika mwaka huu wa kifedha, wizara itasajili na kutoa hati miliki 280,000 za ardhi katika kaunti zote 47.

Waziri Wahome pia alijitolea kugatua huduma za ardhi kwa kufungua afisi nne mpya za ardhi huko Malindi, Kajiado Kusini, Gilgil na Imenti Kusini.

Waziri Karanja alijitolea kuwezesha utoaji wa mbolea ya ruzuku kama njia ya kuimarisha uzalishaji wa mahindi na mazao mengine kote nchini.

Waziri alijitolea kusambaza angalau magunia 12.5 milioni ya mbolea kwa wakulima kufikia mwaka ujao. Wizara pia ilijitolea kusajili wakulima 200,000 zaidi kwenye mfumo wa vocha za kielektroniki.

Chini ya wizara ya Biashara, Waziri Mvurya aliahidi kuratibu utekelezaji wa mpango wa Buy Kenya-Build Kenya.

Wizara pia iliazimia kukamilisha maeneo ya kutengeneza bidhaa za kuuza nje ya nchi na kujenga manne zaidi. Inalenga pia kubuni sera ya biashara ya mtandaoni na mkakati wa huduma za kidijitali.

Kwa upande wake, Waziri Wycliffe Oparanya aliazimia kufuta madeni ya kahawa yenye thamani ya Sh2 bilioni katika mwaka huu wa kifedha na vile vile kushiriki katika maonyesho ya biashara ya kahawa kitaifa na kimataifa ili kukuza zao hilo.

Wizara pia ilijitolea kuongeza upatikanaji wa ufadhili kwa Wafanyabiashara wakubwa, na pia kuwezesha uimarishaji wa mfumo wa utawala na mageuzi ya sera ili kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa wafanyabiashara wakubwa.