Habari za Kitaifa

Ruto: Tutalipia nauli za ndege Wakenya wanaoenda kufanya kazi ng’ambo

Na LUCY MKANYIKA  July 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ameahidi kuwa atawasaidia Wakenya wasiokuwa na kazi kupata ajira ughaibuni huku akilenga kuwatuliza vijana ambao wamekuwa wakimshinikiza ajiuzulu kwa kutotimiza ahadi alizotoa kabla ya kuchaguliwa 2022.

Akizungumza Kaunti ya Taita Taveta, Jumapili, Rais alitangaza kuwa ana mpango wa kuharakisha kutolewa kwa pasipoti kwa wale ambao wanataka kufanya kazi nje ya nchi.

“Nimefanya kazi yangu, nimetafuta kazi mataifa ya nje. Nimepanga kuwa wale ambao wanaenda kufanya kazi hizo ng’ambo wapate pasipoti zao ndani ya wiki moja,” akasema.

“Hata hawatahitaji pesa za kununua tikiti za ndege, tugharimia safari hizo,” akaongeza.

Ahadi yake ilikuja huku Idara ya Uhamiaji ikipambana kuandaa na kuwapa Wakenya pasipoti zao baadhi wakiwa wamesuburi kwa zaidi ya miezi 12.

Kumekuwa na uhaba wa karatasi na mashine za kuchapisha na kuandaa pasipoti hizo. Ufisadi na kiburi kwa wanaofanya kazi kwenye idara hiyo ni kati ya sababu nyingine ambazo zimefanya Wakenya wasipate pasipoti zao kwa wakati.

Mnamo Novemba 2023, Dkt Ruto alisema angetia saini mkataba na serikali za Ujerumani, Ufaransa, Saudi Arabia na mataifa ya Uarabuni ili Wakenya wasiokuwa na ajira wafanye kazi huko.

Hata hivyo, haikubainika ni nafasi ngapi za ajira ambazo zingetokea kutokana na maelewano hayo.

Mnamo Jumapili, Rais alisema serikali imewasaidia zaidi ya vijana 400,000 kupata kazi ng’ambo. Aliwataka wabunge waandae vijana kwenye maeneo yao kujihusisha na mpango wa ajira nje ya nchi.

“Kila wiki vijana 1,000 huhamia nchi za nje. Taita Taveta sasa wanafaa wajiandae kwa zamu yao.

“Kwa wabunge, nimefanya kazi yangu ya kusaka kazi ng’ambo. Nimepanga kuwa kila mtu ambaye angependa kufanya kazi ughaibuni, anapewa pasipoti na stakabadhi nyingine ndani ya wiki moja,” akasema Rais.

Kando na ajira za nje za nchi, Rais alisema kuwa anamakinikia kuanzisha ajira mitandaoni ambapo vijana watafanyia kazi kampuni za mataifa ya nje wakiwa nchini.

“Kwenye mpango wangu nataka vijana wawe na ajira ya maana. Hii ndiyo maana nimeanzisha mipango kama ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, ajira mitandaoni, Wakenya kufanya kazi nje ya nchi, viwanda ili kuwapa vijana wetu ajira ndipo tujenge taifa,” akasema.

Kiongozi wa nchi alifichua kuwa alikuwa amekubaliana na wabunge kujenga vituo vya teknolojia kwa kutumia Hazina ya Fedha ya Kustawisha Maeneobunge Nchini (CDF).

Serikali nayo itanunua kompyuta, kulipia intaneti na kuwalipa wakufunzi kwa vijana ambao watakuwa wakifanya kazi kwa kampuni za ng’ambo na kulipwa dola za Marekani.