Habari za Kitaifa

Sababu za Ruto kumfuta kazi Justin Muturi

Na CHARLES WASONGA March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HATIMAYE Rais William Ruto amempiga kalamu Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi na kumteua Mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku kujaza nafasi yake.

Kwenye taarifa iliyotolewa Jumatano, Machi 26, 2025 na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, kiongozi wa taifa pia amemteua Bi Hanna Wendot Cheptumo kuwa Waziri wa Jinsia na Masuala ya Utamaduni na Sanaa.

“Kwa misingi ya Kipengele cha 152 (2) cha Katiba, watu hawa wawili wameteuliwa kuwa Mawaziri: Hanna Wendot Cheptumo na Geoffrey Kiringa Ruku kama mawaziri wa Jinsia, Utamaduni na Sanaa na Waziri wa Utumishi wa Umma, mtawalia,” Bw Koskei akaeleza kwenye taarifa hiyo.

“Wawili hao wanatarajiwa kuleta katika baraza la mawaziri sio tu uelewa na maarifa ambayo wamepata katika taaluma zao kwa kipindi kirefu bali hekima waliyopata katika safari zao maishani,” akaongeza.

Majina ya Bi Cheptumo na Bw Ruku sasa yatawasilishwa bungeni kupigwa msasa kubaini ufaafu wao kwa nyadhifa hizo muhimu, bunge la kitaifa litakaporejelea vikao vyake Aprili 2, 2025 baada ya likizo fupi.

Wakati huo huo, Rais Ruto pia amefanya mabadiliko ya mawaziri wawili, Aden Duale (Mazingira) na Deborah Barasa (Afya).

Bw Duale sasa atahudumu kama Waziri wa Afya, huku Dkt Barasa akihudumu kama Waziri wa Mazingira.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari/muturi-aendelea-kupapasa-mamba-je-hahofii-kuliwa/

Dkt Ruto amemfuta kazi Bw Muturi saa chache baada ya kumsuta kwa utendakazi mbaya alipohudumu kama Mwanasheria Mkuu kati ya Oktoba 2022 na Julai 5, 2025.

Akiwahutubia viongozi wa dini ya Kislamu katika dhifa ya Iftari katika Ikulu ya Nairobi Jumanne usiku, Dkt Ruto alidai Muturi alilemewa kushughulikia masuala muhimu ya kisheria ikiwemo kuundwa kwa Tume ya Waqf.

Tume hiyo husimamia mali ya kutolewa kama misaada kwa Waislamu wasio na uwezo katika jamii

Kiongozi wa taifa aliihakikishia jamii ya Kiislamu kwamba chini ya Mwanasheria Mkuu wa sasa Dorcas Oduor, atafanikisha kuungwa kwa tume hiyo.

“Nawahakikishia kuwa Tume ya Waqf itaundwa hivi karibuni. Ilifeli kuundwa kwa sababu Mwanasheria Mkuu aliyekuwa wakati ule alikuwa mtepetevu kazini. Mwanasheria Mkuu aliye afisini sasa ni mchapakazi na ataunda tume hiyo haraka iwezekanavyo,” Rais Ruto akasema.

Kiongozi wa nchi pia amemtimua Bw Muturi ambaye pia ni Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa miezi mitatu baada ya Waziri huyo kuihusisha serikali na visa vya utekaji nyara wa Wakenya, haswa vijana, mwaka jana, 2024.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/makala/jamvi-la-siasa/duru-waziri-justin-muturi-hajakanyaga-afisini-kwa-siku-10-sasa/

Mnamo Januari 12, mwaka huu, Bw Muturi alidai kuwa mwanawe, Lesli, alitekwa nyara Juni 2024 na maafisa wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS).

Lesli alihusishwa na maandamano ya Gen Z kukosoa serikali ya Ruto.

Kwenye kikao na wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi, alidai kuwa ilimbidi kumfikia Rais Ruto kwa njia ya simu ndiposa mwanawe akaachiliwa.

“Baada ya Rais kumpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa NIS Noordin Haji ndipo mwanangu aliachiliwa huru. Swali ni je, Wakenya wengine ambao hawana uwezo wa kumfikia Rais watasaidika vipi baada ya watoto wao kutekwa nyara na maafisa wa usalama bila sababu maalum?” akauliza.

Bw Ruku ambaye ameteuliwa kujaza nafasi ya Bw Muturi ndiye Mbunge wa kipekee aliyechaguliwa kwa tiketi ya Democratic Party (DP) katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Muturi alihudumu kama kiongozi wa chama hicho kabla ya kujiuzulu Oktoba 2022 alipoteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu.

Juzi, chama hicho kilitoa notisi ya kutaka kujiondoa kutoka muungano wa Kenya Kwanza, hatua ambayo ilihusishwa na uhusiano hasi kati ya Bw Muturi na serikali ya sasa.