Habari za Kitaifa

Safari ya Uhuru kuwa kinara wa muungano mpya Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI September 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KONGAMANO la Limuru III lilikuwa na ajenda yenye vipengele kumi na baadhi ya ajenda hizo zilitimia siku za hivi karibuni.

Viongozi wa upinzani katika eneo la Mlima Kenya wanasema ajenda yao ya kutaka Rais mstaafu Uhuru Kenyatta aongoze muungano mpya wa kisiasa iko katika hatua ya kutekelezwa.

Kadhalika wanasema maandamano ya hivi majuzi ya vijana wanaopinga serikali yalitimiza sehemu ya mikakati yao.

Hii ni licha ya shughuli chache za kisiasa kutoka kwa rais huyo mstaafu waliyemtangaza kuwa kiongozi wa Muungano wao mpya wa Haki.

Huku wakiapa kuendelea na azimio lao la kukosoa Kenya Kwanza kwa utawala mbaya, wanasema vijana walioandamana, hasa wa Gen-Z, waliozaliwa kati ya 1996 na 2012, na kuondolewa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 ni ushindi mkubwa kwa harakati zao.

Waandalizi wa kongamano hilo wanasema kwamba hawajalegea licha ya matokeo ya maandamano hayo, wakisisitiza kuwa ajenda yao kuu ya kumfungia nje Rais William Ruto kutoka eneo ambalo lilimpa asilimia 87 ya kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 inaendelea vyema.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni, vijana ambao hawakufurahishwa na serikali ya Rais William Ruto, wanaibua masuala waliyoyajadili kwenye kongamano hilo.

Aliandaa hafla ya Limuru III mnamo Mei 17, 2024 akiwa na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu Wachira Kiago miongoni mwa wengine.

‘Sasa tunaweza kusema kwamba tuliunga mkono maandamano ya Gen Z kimyakimya, yalikuwa sehemu ya mpango wetu na yalitusaidia kufikia baadhi ya malengo ya ajenda kama vile kuondolewa kwa Mswada wa Fedha wa 2024,’ alisema.

Bw Kioni na Bi Karua katika miezi ya hivi majuzi pia wamekuwa miongoni mwa wakosoaji wakuu wa kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga, ambaye amekuwa akimpigia debe Rais William Ruto.

Aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Elimu Zack Kinuthia, ambaye aliunga mkono Limuru III, anasema kuwa mkutano huo ulitayarisha mazingira ya maandamano yaliyoshuhudiwa.

‘Ulikuwa ni mkusanyiko wa watu ambao walisikiliza kwa makini,’ asema Bw Kinuthia.

Hata hivyo, anasema wazo la Muungano wa Haki halikufikiriwa vyema na tangazo hilo liliwashangaza wengi.

Ingawa Narc Kenya ya Bi Karua imetangaza nia ya kuondoka Azimio kufuatia baadhi ya washirika wa Bw Odinga kuteuliwa mawaziri katika serikali ya Rais Ruto, Bw Kioni alisema “tuko imara na makini zaidi kuliko hapo awali.”

Bi Karua kwa upande wake aliambia Taifa Leo kwamba “nia ya kuondoka Azimio haimaanishi kwa vyovyote vile kuacha kutafuta Kenya yenye haki ambapo utawala wa sheria ni tukio la kawaida na kuanzishwa kwa serikali inayoheshimu matakwa na maadili ya kitaifa.”

Alisema Muungano wa Haki ambao ulipangwa kuleta pamoja vyama 31 vya kisiasa nchini ndio msingi wa mashambulizi dhidi ya utawala wa Rais Ruto.