Sakata ya mbolea feki yasababisha Sweden kukanyagia msaada wa Sh513 milioni
SAKATA ya mbolea feki iliyotikisa serikali mapema mwaka huu imenyima kaunti zaidi ya Sh513 milioni kutoka kwa mashirika ya ufadhili, Bunge limeelezwa.
Serikali ya Uswidi imefutilia mbali Sh513.2 milioni zilizodhamiriwa kuimarisha kilimo katika kaunti kufuatia sakata hiyo ya mbolea.
Kamati ya Seneti kuhusu Ushikamano, Nafasi Sawa na Utangamano Kimaeneo ilisikia kuwa kila kaunti imepoteza Sh10.9 milioni baada ya ufadhili kufutiliwa mbali.
Sweden ilikuwa imepatia Kenya Sh513,189,193 kama ufadhili unaoambatana na masharti kwa serikali za kaunti chini ya Mradi wa Maendeleo ya Kilimo na Biashara Uswidi-Kenya (KABDP).
Fedha hizo zilijumuishwa katika Mswada wa Fedha za Ziada zinazoambatana na masharti kwa Kaunti 2024, lakini mfadhili ameondoa msaada wake.
Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo alieleza Kamati hiyo kuwa serikali ya Sweden ilifutilia mbali ufadhili wake kutokana na sakata ya mbolea iliyoyumbisha Wizara ya Kilimo.
“Nilikutana majuzi na Balozi wa Sweden nchini aliyenieleza kuwa miradi ya kaunti iliyo chini ya KABDP 2 imefutiliwa mbali kutokana na sakata ya mbolea iliyokumba serikali kuu,” alisema Bw Kilonzo.
“Mambo tunayofanya katika kiwango cha serikali kuu yanaathiri kaunti kwa njia kubwa. Sakata ya mbolea imeathiri fedha za wafadhili. Bajeti za kaunti hadi asilimia 40 hufadhiliwa na hela za wahisani,”
Bw Kilonzo Jn alifichua haya alipofika mbele ya Kamati ya Ushikamano inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Mandera, Mohammed Chute, iliyochunguza ujumuishaji wa waajiriwa wote wa serikali ya Kaunti ya Makueni.
Mnamo Mei, aliyekuwa waziri wa kilimo, Mithika Linturi alinusurika hoja ya kumtimua iliyowasilishwa na Mbunge wa Bumula, Jack Wamboka, kuhusu madai matatu yaliyomhusisha waziri na mbolea feki katika mpango wa serikali.
Bw Linturi aliponea chupuchupu mswada huo wa kumfurusha baada ya kamati maalum kubaini kuwa madai hayo hayakuwa na msingi.
Bw Wamboka aliwasilisha mswada wa kumtimua waziri kwa misingi mitatu ikiwemo ukiukaji wa katiba, sababu thabiti ya kuamini kuwa waziri alikuwa ametenda hatia chini ya sheria za nchi na ukosefu wa nidhamu.
Bunge la kitaifa kupitia kamati maalum lilimwondolea maovu yote Bw Linturi katika sakata hiyo iliyohusu kuwauzia mbolea ghushi wakulima chini ya mpango wa mbolea ya bei nafuu uliofadhiliwa na serikali.
Wanachama saba wa kamati hiyo yenye wanachama 11 walipiga kura kumwokoa Bw Linturi asifurushwe.
Kamati hiyo iliongozwa na Mwakilishi Mwanamke Kaunti ya Marsabit, Naomi Waqo, na ilibuniwa kuchunguza misingi kuhusu hoja ya utimuaji iliyowasilishwa na Bw Wamboka.
Kamati hiyo iliafikiana kwa pamoja kuwa mbolea ghushi ilinunuliwa na kuuzwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Nchini (NCPB).