Sekta ya utalii yazidi kuimarika licha ya usalama kudorora
SEKTA ya utalii inatazamiwa kukua mwaka huu na kuletea nchi zaidi ya Sh560 bilioni kufuatia kuwasili kwa maelfu ya wageni kupitia meli na ndege licha ya wasiwasi kuhusu usalama.
Waziri wa Utalii, Rebecca Miano, alihakikishia watalii wanaotembelea Kenya kuhusu usalama wao, huku Amerika ikitoa onyo kwa raia wanaozuru Kenya kuepuka baadhi ya sehemu.
Waziri Miano anasema serikali imeweka mikakati kuhakikisha usalama wa wageni katika mpango wake wa mwaka wa kuvutia angalau wageni milioni 3.
“Tunataka kuwahakikishia wageni wetu kwamba wanaweza kutembea kwa uhuru, wajihisi salama, na mikakati ya kutosha imewekwa ili kuhakikisha usalama wao,” alisema Waziri Miano.
Jumanne wiki jana, Amerik ilitangaza baadhi ya maeneo ya pwani na kaskazini mwa Kenya kuwa hatari na kuonya raia wake kutoyatembelea.
Hata hivyo, Miano alisema serikali imeweka mipango kuhakikisha usalama wa watalii Pwani, ambayo inachangia takriban asilimia 50 ya mapato ya sekta ya utalii.
Alisema kwamba inakadiriwa watalii wa kimataifa mwaka huu watakuwa 3 milioni na idadi inatarajiwa kuongezeka hadi 5 milioni katika miaka miwili ijayo.
Mwaka 2024, sekta ya utalii ya Kenya iliimarika kwa kasi, huku mapato ya utalii yakiongezeka kwa asilimia 19.79 hadi Sh452.20 bilioni.
Mapato kutoka watalii wa kigeni yaliongezeka kutoka Sh377.49 bilioni mwaka 2023, hadi Sh452.20 bilioni mwaka 2024.
Kenya ilikaribisha watalii 2.4 milioni wa kimataifa mwaka 2024, ongezeko la asilimia 15 kutoka milioni 2.09 mwaka 2023.
Ukuaji huu unahusishwa na juhudi za masoko ya kimkakati, utoaji wa bidhaa mbalimbali za utalii, na kuanzishwa kwa safari mpya za ndege.
Serikali inajikita katika kuboresha majukwaa ya kidijitali na kuboresha uzoefu wa wageni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.