Habari za Kitaifa

Serikali kununua gunia la mahindi kwa Sh4000 kinyume na matarajio ya wakulima ya Sh6000

Na TITUS OMINDE September 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI itanunua mahindi kutoka kwa wakulima kwa Sh4,000 sawa na bei ya mwaka wa 2023, ingawa wakulima walitarajia bei ya Sh6,000, Katibu wa wizara ya Kilimo Paul Ronoh amesema.

Ripoti ya Jopo la Kusimamia Utoshelevu wa Chakula Kenya (KFSSG) na Wizara ya Kilimo inatabiri mavuno ya mahindi ya tani 4.2 milioni mwaka wa 2024, ongezeko kubwa la asilimia 15-20 ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Wizara ya Kilimo iliripoti kuwa nchi ilizalisha magunia 61 milioni mwaka 2023 kwa sababu ya hali nzuri ya hewa na mpango wa mbolea ya ruzuku.

Mwaka huu wa 2024, nchi inatarajia magunia 80 milioni ya mahindi.

Katibu wa wizara ya Kilimo Paul Ronoh amewapongeza wakulima kwa kujitolea kwao kuhakikisha utoshelevu wa chakula nchini, na kutangaza kuwa mwaka huu, serikali itanunua mahindi kutoka kwa wakulima kwa Sh4,000.

Bw Ronoh alisema bei ya serikali kwa wakulima ndiyo bora zaidi katika soko la kimataifa, akiwataka wakulima kubadilisha mazao yao ili kupata faida kubwa zaidi.

Hata hivyo, aliwataka wakulima wasioridhika na bei ya serikali kutafuta masoko mengine kwa bei ya juu ya mazao yao.

‘Hatutamlazimisha mkulima yeyote kuuza mazao yake kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) ikiwa anahisi kuwa anaweza kuuza mahali pengine kwa bei nzuri zaidi ya ile ambayo serikali itakuwa ikitoa mwaka huu,’ Katibu aliambia wakulima alipozuru mabohari ya NCPB katika eneo la North Rift.

Aliagiza bodi ya nafaka kuharakisha na kuuza akiba ya zamani ya mahindi waliyonayo kabla ya wakulima kuvuna mazao yao katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, huku kukiwa na ongezeko la uzalishaji wa mahindi mwaka huu kutokana na hali nzuri ya mvua.

Bw Ronoh aliyeandamana na Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii na Mbunge wa Kesses Julius Ruto alisema serikali inathamini jukumu la wakulima katika utoshelevu wa chakula, na itaendelea kutoa ruzuku kwa bei ya mbolea na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo muhimu za kilimo kwa wakati.

Katibu Rono ilifichua kuwa vikaushio vinavyohamishika vitatolewa kwa wakulima ili kudhibiti hasara baada ya kuvuna, na akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kwa kuweka mazao yao kwenye mabohari yaliyopo ili wapate risiti ghalani.

“Uvunaji wa mahindi katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa na eneo la Magharibi huanza katikati ya Oktoba na Novemba. Ninataka bodi kuharakisha kuondoa ya zamani ili kutoa nafasi kwa mazao mapya,” alisema.