Serikali kuwalipa mabilioni madaktari waliopambana na corona
WIZARA ya Afya itawalipa Sh6.3 bilioni kama marupurupu madaktari zaidi ya 8,000 waliokuwa mstari wa mbele kupambana na janga la Covid-19 lakini hawana kazi kwa sababu serikali imefeli kuwaajiri.
Baada ya kutoswa huku na kule kwa miaka kadhaa, madaktari hao 8,442 watapokea jumla ya Sh6,300,385,920 kama kiinua mgongo baada ya serikali za kaunti kukataa kuwajumuisha kwenye ajira ya kudumu.
Covid-19 ilipozuka 2020, serikali iliwaajiri matabibu 8,571 wanaojumuisha madaktari, wauguzi, maafisa wa kliniki na wataalam wa maabara kupitia kandarasi za miaka mitatu chini ya Mpango wa Afya Bora kwa Wote (UHC).
Walitumwa hospitali za umma katika kaunti 47 kusaidia wagonjwa wa Covid-19 kwa ahadi kwamba wangejumuishwa katika ajira ya kudumu.
Wiki tatu zilizopita, serikali kuu iliwaajiri madaktari 108 huku serikali za kaunti zikitarajiwa kuajiri waliosalia. Baadhi yao wamefariki dunia katika muda huo.
Madaktari hao hulipwa kati ya Sh40,000 hadi Sh50,000 kila mwezi.
Serikali za kaunti, hata hivyo, zimekataa kuajiri kundi hilo zikitaja changamoto za kifedha.
Naibu Mkurugenzi wa afya katika Wizara ya Afya, Dkt Sultani Matendechero, amesema ikiwa serikali za kaunti hazitawaajiri wafanyakazi, mpango huo utakatizwa baada ya muda wa kandarasi zao kukamilika.
“Ikiwa kaunti zitakataa kuwaajiri hatutakuwa na hiari ila kuwalipa marupurupu kisha tuwarudishe nyumbani,” alisema Dkt Matendechero.
Jopokazi lilipendekeza afua mbili: kuajiri kundi hilo kwa gharama ya Sh7.7 bilioni au kuwalipa marupurupu yatakayogharimu Sh6.3 bilioni.
Tume ya Huduma ya Umma (PSC) iliruhusu kandarasi mpya kwa wafanyakazi wa
UHC mnamo Mei 17, 2023.
Oktoba 8, Baraza la Magavana (CoG) lilimwandikia Katibu wa Wizara ya Afya Mary Muthoni, kuhusu mvutano kwenye ‘uhamisho wa wahudumu wa afyia chini ya shirika la Global Fund.’
Afisa Mkuu wa CoG, Mary Mwiti, alibatilisha muafaka kati ya Kenya na Global Fund uliotekelezwa na Hazina ya Kitaifa uliohitajika kuwaajiri maafisa wa afya kupitia ufadhili wa Global Fundkama sehemu ya ustawishaji kufikia Disemba, 2023.
“Inasikitisha kuwa serikali kuu iliahidi na kutekeleza muafaka unaozidisha majukumu ya kifedha kwa serikali za kaunti pasipo kujadiliana au kutengea serikali za kaunti fedha zinazohitajika kutekeleza majukumu hayo. Bila kutoa pesa zinazohitajika, serikali za kaunti huenda zikashindwa kuwaajiri wafanyakazi wa Global Fund,” alisema Bw Mwiti.
Aprili mwaka huu, Bi Muthoni alisema jopokazi linalojumuisha mashirika mbalimbali ikiwemo hazina kuu, PSC, Wizara ya Afya na CoG, zilibaini kuwa haiwezekani tena kwa wahudumu wa UHC kuendelea kuhudumu kupitia kandarasi kwa sababu maafikiano yanakiuka sheria kuhusu ajira.
“Jopokazi pia lilibaini kuwa gharama ya kuwaajiri wafanyakazi wa UHC kwa mkataba wa kudumu ni Sh 7,747,802,365 zinazojumuisha Sh 4,238,452,404 ambazo zipo kwenye bajeti ya serikali kuu,” alieleza Katibu wa Wizara.