Habari za Kitaifa

Serikali: Vijana kupoteza matumaini ni chanzo cha kuingilia uhalifu

Na GEORGE ODIWUOR September 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WIZARA ya Usalama wa Ndani imetaja ukosefu wa nafasi za kujiendeleza kiuchumi, kupotoshwa na wenzao na kupoteza matumaini maishani kama sababu kuu zinazochangia vijana kujiingiza katika uhalifu.

Katibu katika Wizara hiyo Raymond Omollo alisema matumizi ya pombe na dawa za kulevya pia huchangia vijana kujihusisha na vitendo vya uvunjaji sheria.

Miongoni mwa vitendo hivyo ni wizi, ulaghai, uteketezaji mali na wizi wa mabavu.

Dkt Omollo hata hivyo alitaja uhalifu wa mitandao kama suala kuu huku idadi ya waathiriwa ikiongezeka kufuatia ongezeko la uhalifu huo wa mitandaoni.

Baadhi ya vitisho hivyo, akasema, vinaendelezwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

“Uhalifu wa mitandaoni una madhara makubwa kwa afya ya kiakili ya vijana,” Dkt Omollo akasema.

Wizara ya Usalama wa Ndani pia imeelezea hofu kwamba maambukizi ya Ukimwi, mimba za mapema miongoni mwa vijana na Dhuluma za Kijinsia (GBV) pia ni tishio kubwa kwa vijana nchini.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) la 2022, inakadiriwa kuwa idadi ya vijana nchini itaongezeka hadi milioni 16.915 mnamo 2025, milioni 18.036 mnamo 2030 na milioni 18.966 mnamo 2035.

Dkt Omollo alisema serikali ina wajibu mkubwa wa kukabiliana na changamoto zinazowaathiri vijana.

Alisema hiyo inaweza kufanyika kupitia kuimarishwa kwa juhudi za kupambana na pombe haramu na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

“Wajibu huu unahusu pakubwa uwekaji wa mikakati ya uzuiaji, kuwazuia na kuwafundisha waathiriwa,” Katibu huyo wa wizara akaeleza.

Dkt Omollo pia alisema serikali imejitolea kuzima kabisa dhuluma za kijinsia kufikia mwaka wa 2026.