Habari za Kitaifa

SHIF ni balaa tele, vilio vya mateso vyazidi huku serikali ikiitetea

Na SAM KIPLAGAT October 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAGONJWA wanaendelea kuteseka wakisaka matibabu chini ya Hazina ya Afya ya Jamii (SHIF) huku daktari mtaalamu wa upasuaji akianika masaibu ambayo Wakenya wamekuwa wakipitia tangu mpango huo ulipoanza kutumika mnamo Oktoba 1.

Tangu uanze kutumika, kumekuwa na kilio kutoka kwa Wakenya ambao wamelazimika kugharimia matibabu kutoka kwa mifuko yao kutokana na changamoto zinazoandama SHIF.

Akiwasilisha malalamishi yake kwenye kesi ya kupinga bima hiyo mpya akiwa hospitalini kwa njia ya mtandao, Dkt Magare Gikenyi alisema hangeweza kufanyia mgonjwa upasuaji kwa sababu ya kufeli kwa SHIF.

Hii ni licha ya kuwa, alikuwa amelipa ada zote chini ya Bima ya zamani ya NHIF ambayo matumizi yake yaliisha mwishoni mwa Septemba. Mtaalamu huyo alisema haikuwa haki kwa watumishi wa umma na mwanachama wa Muungano wa Madaktari na Matabibu Nchini (KMPDU) kama yeye kuruhusiwa kuendelea kutumia NHIF huku Wakenya wakiachwa kivyao na kutakiwa kutumia SHIF.

“Kuna matukio mengi Jaji. Sisi tumeruhusiwa kutumia NHIF hadi Novemba 30 kwa sababu tulipiga kelee ilhali Wakenya wameachwa kivyao bila mtu wa kuwatatea na wanaendelea kuhangaika wakisaka matibabu, wengine hata wakifa,” akasema Dkt Gikenyi.

Mtaalamu huyo alitoa wito kwa mahakama isimamishe SHIF hadi kesi ambayo amewasilisha pamoja na watu wengine wawili isikizwe na iamuliwe.

Jana, wagonjwa nao waliendelea kuhangaika baada ya SHIF kukosa kufanya kazi kwenye Hospitali ya Kenyatta na ile ya Rufaa na Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTTRH).Walilia baada ya kukaliwa kulipia huduma ambazo awali zilikuwa zikigharimiwa na NHIF.

Wagonjwa ambao walikuwa wamefika KUTRRH na kusaka huduma za kusafishiwa damu walitakiwa walipe Sh4,600 huku usimamizi wa hospitali hiyo ukisema kuwa, kiwango ambacho kimetengwa na SHIF kwa matibabu hayo ni kidogo sana ikilinganishwa na ilivyokuwa chini ya NHIF.

Katika hospitali ya Kenyatta, wagonjwa walishindwa kulipa pesa za matibabu yao kwa sababu SHIF haikuwa ikifanya kazi huku wengi wao wakionyesha kero zao na mfumo huo mpya.

Huku wagonjwa wakiendelea kuteseka, serikali kupitia Wizara ya Afya nayo ilitetea SHIF ikisema, tatizo katika kukumbatiwa kwa bima hiyo mpya ni malipo wala si mtandao wake kufeli kufanya kazi.

Kupitia wakili Kioko Kilukumi, wizara hiyo ilisema ilikuwa imetumia Sh4.5 bilioni kulipa vituo vinavyotoa huduma za kimatibabu ili wagonjwa wasitatizike na wahudumiwe ipasavyo.

Bw Kilukumi alisema mtandao unaotumika na SHIF unawarahishia kazi wale ambao wamesajiliwa wanapopokea huduma za kimatibabu. Kufikia Oktoba 28 Wakenya 13,338,143 walikuwa wamesajiliwa na bima hiyo mpya kwa mujibu wa Bw Kilukumi.

Hospitali na vituo vya afya 7,563 vimekuwa vikiwapokea na kuwahudumia wagonjwa ambao wamejisajili na SHA. Kwa hivyo, asilimia 96.1 za vituo vya kiafya ambavyo vina leseni vimekuwa vikitoa huduma za SHIF kulingana na wizara ya afya.

Wizara iliongeza kuwa, gharama inayotokana na maombi 88, 244 ya kusaka matibabu ambayo ni Sh1.4 bilioni yalikuwa yamewasilishwa kwenye mtandao wa SHIF na tayari maombi 38,200 yalikuwa yameidhinishwa.

Bw Kilukumi pia alisema vituo 3,023 vya afya vilikuwa vimeidhinisha maombi 114,034 ya wagonjwa ambao wanahitaji huduma za matibabu na wakatibiwa.

“Mtandao au tovuti ya bima hii mpya haina tatizo lolote. Shida ambayo ipo inatokana na malipo na wengi sasa hawana tatizo la kupata huduma za afya,” akasema Bw Kilukumi.

Wakili huyo pia aliomba mahakama iharakishe kusikizwa kwa kesi hiyo ili ikamilishwe kwa muda mfupi. Kesi hiyo itasikizwa mnamo Novemba 22.

Dkt Gikenyi na Seneta wa Busia Okiya Omtata na Eliud Matindi wote wamepinga SHA wakisema kuwa tangu ianze kutumika, wagonjwa wamekuwa wakipitia mahangaiko makubwa.

Watatu hao wanasema wagonjwa wamekuwa wakikosa huduma za matibabu na kulazimishwa walipe pesa kutokana na mtandao wa SHIF kukosa kufanya kazi baada ya kuondolewa kwa NHIF.

Wanasema itachukua Safaricom zaidi ya miaka miwili kuhakikisha kuwa mtandao ambao ni msingi wa huduma zinazotolewa na SHA, unafanya kazi kikamilifu jinsi ilivyokuwa kwa NHIF.