Shughuli tele zasubiri Wabunge kufanikisha mageuzi ya Ruto
WABUNGE watakabiliwa na shughuli nyingi watakaporejelea vikao Julai 23, kwani mabadiliko kadha yanayofanywa na Rais William Ruto sasa yanahitaji mchango wao.
Kuanzia Mswada wa Fedha wa 2024 uliokataliwa, mapendekezo ya kupunguzwa kwa bajeti, kupigwa msasa kwa mawaziri wapya baada ya kufutwa kwa mawaziri 21 na kujadiliwa kwa mswada wa kudhibiti michango ya harambee.
Aidha, wabunge hao watapiga msasa Inspekta Jenerali mpya wa polisi kufuatia kujiuzulu kwa Japhet Koome na kujadili miswada minane ya kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco).
Kimsingi, wabunge watakuwa na kibarua cha kufanikisha utekelezaji wa mabadiliko makubwa yanayohitajika serikali ili itimize matakwa ya vijana wa Gen-Z.
Wakati huu, Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Fedha inashughulikia upya mswada huo tata wa fedha uliokataliwa na Wakenya na inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake bungeni wakati wowote kuanzia Julai 23.
Hii ni baada ya Rais William Ruto kukataa kutia saini mswada huo baada na vijana hao kuandaa msururu wa maandamano kuupinga.
Baada ya hapo bunge litapewa muda wa siku 21 kujadili na kupitisha ripoti hiyo na kuipigia kura.
Ikiwa wabunge watakubaliana na mapendekezo ya Rais, kwamba sehemu zote 79 ya mswada huo zifutuliwe mbali, ina maana kuwa serikali itaendelea kukusanya ushuru kwa kutumia Sheria ya Fedha ya 2023.
Tayari Hazina ya Kitaifa imewajulisha maafisa wakuu katika Wizara, Idara na Mashirika ya Serikali Kuu kwamba baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 wanapaswa kufutulia mbali miradi yote mipya iliyoratibiwa kutekelezwa katika mwaka huu wa kifedha wa 2024/2025.
Hii ni kwa sababu serikali inapanga kupunguza mgao wa bajeti kwa asasi hizo kufuatia pengo lililosababishwa na kukataliwa kwa mswada huo ambao ungeisaidia serikali kukukusanya Sh347 bilioni zaidi.
Tayari Rais Ruto ametangaza mikakati mingine ya kupunguza matumizi ya fedha serikalini ambayo itahitaji kujadilishwa na kuidhinishwa na wabunge.
Kwa mfano, kiongozi wa taifa ametangaza kuwa serikali itafutulia mbali au kuunganisha mashirika 47 ya serikali ambayo majukumu yake yanafanana.