Siasa zakosa kuporomoshwa makanisani kwa mara ya kwanza katika historia
HAKUNA siasa zilizoporomoshwa makanisani Jumapili kutokana na “marufuku” iliyowekwa na vijana wa Gen-Z na iliyotekelezwa kikamilifu na viongozi wa makanisa hayo.
Haya yalifanyika tu huku vijana na makanisa wakiendelea kukashifu utawala wa Rais William Ruto kutokana na mapendekezo mengi ya ushuru ambao upo katika Mswada wa Fedha 2024.
Mnamo Ijumaa vijana hao ambao wamekuwa wakiandamana kupinga Mswada tata wa Fedha wa 2024 waliapa “kuteka makanisa” na kuzima mienendo ya wanasiasa kuyageuza kuwa majukwaa ya kuchapa siasa kila Jumapili.
Walikasirishwa haswa na wabunge 204 ambao mnamo Alhamisi walipiga kura ya kuunga mkono mswada huo na kuuvukisha hadi hatua ya kushughulikiwa kwa awamu ya tatu.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Nchini Jackson Ole Sapit alikuwa wa kwanza kutekeleza takwa la Gen-Zs alipozima ombi la Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba mbunge mmoja ahutubie waumini katika Kanisa la Kianglikana mjini Nyahururu, kaunti ya Laikipia.
Fursa ya kipekee ambayo Bw Gachagua alipewa ni ile ya kusoma majina ya takriban wabunge 30 waliofika hapo kuhudhuria hafla ya kutawazwa kwa Askofu mpya Samson Mburu wa jimbo la Nyahururu.
Kisha, alinena machache kabla ya kumwalika Rais William Ruto awahutubie waumini.
“Idadi ya wabunge waliofika kuungana nasi katika hafla hii ni kubwa mnamo. Kwa hivyo, Askofu Mkuu naomba nimpe mmoja wao nafasi kidogo ya kusalimia watu wa Mungu,” Bw Gachagua akamuomba Ole Sapit.
“Haya, sawa nitaheshimu uamuzi wako Baba Askofu Mkuu,” Bw Gachagua akasema, ishara ya kusalimu amri baada ya Askofu huyo Mkuu kukatalia mbali ombi lake.
Baadaye, Naibu Rais alijikita katika masuala ya kuwahimiza waumini kudumisha umoja huku akitoa wito kwa viongozi kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Rais atoa hotuba fupi isiyozidi dakika 20
Kwa upande wake, Rais Ruto alitoa hotuba fupi ambayo haikuzidi dakika 20, ambapo alielezea kujitolea kwa serikali kushughulikia matakwa ya vijana hao.
“Ninaheshimu uamuzi ambao vijana wamechukua kuhakikisha kuwa malalamishi yao yanashughulikiwa. Lakini sharti amani idumishwe nchini. Masuala yaliyoibuliwa na vijana yatashughulikiwa kikamilifu. Nitafanya mazungumzo nao ili kuangazia masuala waliyoibua,” Bw Ruto akasema.
“Mswada wa Fedha wa 2024 utaangazia changamoto zinazowakumba vijana hawa kwani tumetenga fedha zaidi kwa Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge zitakazotumiwa kuanzisha vituo vya kidijitali vitavyotumiwa na vijana kupata ajira mitandaoni.
Vile vile, tuneongeza mgao wa fedha kwa Bodi ya Hazina ya Kufadhili Masomo ya Vyuo Vikuu (HELB) ili hata vijana kutoka familia maskini wapate nafasi ya kusoma,” Dkt Ruto akaongeza.
Wanasiasa wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na magavana; Joshua Irungu (Laikipia), Dkt Kiarie Badilisha (Nyandarua) na Seneta wa Nyandarua John Methu.
Nao wabunge walikuwa Faith Gitau (Mbunge Mwakilishi wa Nyandarua) Jane Kihara (Naivasha) John Kiarie (Dagorreti Kusini) na Mwangi Kiunjuri (Laikipia Mashariki).
Katika Kanisa Katoliki la Holy Family Basilica na Kanisa la Kianglikana la (ACK) la All Saints Cathedral, hakuna wanasiasa walipewa nafasi ya kutuhubia waumini.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nairobi Philip Anyolo alisema kanisa hilo linawachukulia wanasiasa kama waumini wa kawaida na kamwe haliwezi kuwapa nafasi ya kipekee kuwahutubia waumini.
“Huo ndio umekuwa msimamo wetu nyakati zilizopita na hata sasa. Hata hivyo, kanisa hili linasimama na waandamanaji wanaotekeleza haki yao ya kikatiba,” akasema.
“Polisi wanafaa kuruhusu makundi ya kutoa huduma za kwanza kuwafikia wale ambao huenda wakajeruhiwa,” akaongeza Askofu Mkuu Anyolo.
Idadi kubwa ya vijana hao walihudhuria ibada ya jana na kuapa kuendelea na maandamano yao ya kupinga Mswada wa Fedha.
Baadaye waliungana na wenzao waliodhuhuria ibada katika makanisa mengine na kufanya maandamano ya amani katika barabara kadhaa za jiji la Nairobi.
Hakukutokea patashika yoyote kwani polisi hawakujaribu kuwatawanya kwa vitoa machozi.
Ripoti za Waikwa Maina, Kevin Cheruiyot na Hillary Kimuyu