Sijaiba chochote, Gachagua ajitetea vikali
NAIBU Rais Rigathi Gachagua amejitetea vikali dhidi ya mashtaka dhidi yake yaliyomo kwenye hoja ya kumtimua afisini akiyataja kama yasiyo na msingi wowote.
Amepinga madai ya Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, ambaye ni mdhamini wa hoja hii, kwamba amejilimbikizia mali ya thamani ya Sh5.2 bilioni.
Hii anasema ni kinyume na mapato yake yanayojulikana, kupitia mshahara wake wa miaka miwili, wa Sh24 milioni.
Kwenye kikao na wanahabari katika makazi yake mtaani Karen Jumatatu, Nairobi, Bw Gachagua alifafanua kuwa mkahawa wa Olive Garden Hotel na mkahawa wa Vipingo Beach Hotel, ulioko Malindi, Kaunti ya Kilifi ni mali ya kakake mkubwa Gavana wa zamani wa Nyeri marehemu James Nderitu Gachagua.
“Mimi, Mwai Mathenge ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ujenzi na Njoroge Regero ambaye ni wakili tuliteuliwa na marehemu kakangu kuwa wasimamizi wa mali hizi. Mkahawa wa Olive Garden uliuzwa kwa Sh450 milioni na pesa hizo zikagawiwa watoto wa marehemu kakangu, Gavana wa zamani James Nderitu Gachagua,” akasema.
Bw Gachagua pia alikana madai kuwa alinyakua ardhi ya ukubwa wa ekari 40 katika eneo bunge la Kieni, akisema alinunua ardhi hiyo kutoka kwa Mbunge wa eneo hilo Njoroge Wainaina.
“Nashangaa Bw Wainaina ni miongoni mwa wabunge waliotia saini hoja ya kuniondoa afisini ilhali anafahamu fika kwamba ndiye aliyeniuzia kipande hicho cha ardhi ambacho ukubwa wake halisi ni ekari 35,” Bw Gachagua akasema.
Vile vile, alifafanua kuhusu vipande vya ardhi ambavyo anamiliki katika eneo la Mathira Magharibi na Kaunti ya Meru, akisema hiyo ni mali aliyonunua kabla ya kuingia afisini kama Naibu Rais.
Bw Gachagua pia alipinga madai anamiliki mkahawa wa Oustpan na mkahawa wa Treetop kupitia wanawe wawili.
“Mikahawa hii miwili inamilikiwa na watoto wangu ambao ni watu wazima na ambao wako huru kufanya biashara kama Wakenya wengine. Na mikahawa hii na kampuni zingine zinazomilikiwa na watoto wangu hazijawahi kufanya biashara na serikali,” akaeleza.
Bw Gachagua alisema kuwa Jumanne atafika bunge kujitetea vikali dhidi ya madai hayo na mengine yaliyoko kwenye hoja hiyo. Alisema Wakenya milioni 7.1 waliomchagua na Rais William Ruto wako na haki ya kusikia utetezi wake bungeni kwa sababu “wao ndio wenye mamlaka makuu kulingana na kipengele cha kwanza cha Katiba.”