Habari za Kitaifa

Sikusaliti yeyote kuridhiana na Ruto, niko na mpango, asema Raila

Na KASSIM ADINASI May 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, ametetea maridhiano yake na Rais William Ruto yaliyopelekea kuundwa kwa serikali jumuishi, akisisitiza kuwa hayakuwa usaliti kwa mtu yeyote au kikundi chochote nchini Kenya.

Akihutubu katika mazishi ya mwandishi mkongwe Edward Kwach katika Kaunti Ndogo ya Ugunja, Bw Odinga alisema hakuna mtu anayepaswa kulalamika kuhusu maridhiano hayo.

Kauli yake inajiri kufuatia ukosoaji kwamba alisaliti kizazi cha vijana wa Gen Z kwa kujiunga na Rais Ruto wakati ambao kiongozi wa nchi alikuwa amebanwa kisiasa.

Chama cha ODM, kimekumbwa na misukosuko ya kisiasa, kikigawanyika baina ya wanaounga mkono na wanaopinga muafaka wa kisiasa na serikali ya Kenya Kwanza.

“Watu wanalalamika kuhusu maridhiano yangu na Rais Ruto. Maridhiano si kitu kibaya. Sijawahi kuwa na maridhiano ya kumsaliti mtu wangu,” alisema kiongozi huyo wa ODM.

Bw Odinga alieleza kuwa maridhiano hayo ya kisiasa yalilenga kumpa yeye na wafuasi wake mwelekeo mpya wa kisiasa.

“Unapoona mawingu yakikusanyika angani, jua natafuta mwelekeo wa kisiasa unaofaa kwa ajili ya watu. Upepo unapovuma sana, jua mvua inakaribia kwa sababu najua tunakotaka kuelekea,” alisema.

Akikumbuka Uchaguzi Mkuu wa 2022 ambao alishindwa na Rais Ruto, alikiri kuwa kulikuwa na changamoto.

“Tulikuwa tumepata mwelekeo, lakini ikawa hivyo. Waswahili husema yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Tuna mpango,” aliongeza.

Alisisitiza kuwa matukio ya kisiasa yanayoendelea nchini hayafai kuwatia wasiwasi wafuasi wake.

“Mambo yanayoendelea kisiasa yasiwatie hofu. Tunajua tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Kama mechi ya kandanda, tunafanya mazoezi uwanjani lakini tunaelewa lango liko wapi,” alisema.

Chama cha ODM kimeendelea kushuhudia mvutano wa kisiasa, upande mmoja ukiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna na Gavana wa Siaya James Orengo, huku upande mwingine ukiunga mkono muafaka wa kisiasa na serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Sifuna amekuwa akipinga wazo la “serikali jumuishi” akisema hakuna kitu kama hicho: “Kuna serikali moja tu ya Kenya Kwanza.”

Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi, hivi karibuni alimkosoa Gavana Orengo katika hafla huko Ugunja, akimtaka aachane na siasa za uanaharakati na aelekeze nguvu kwa maendeleo ya kaunti.

“Gavana lazima aelekeze nguvu kwa utoaji wa huduma na aache kuwa mwanaharakati ilhali ana mamlaka ya kuhudumia watu akiwa ofisini,” alisema Wandayi mbele ya waombolezaji.